Header Ads Widget

NCHIMBI AMPONGEZA LUKUVI KWA MIRADI YA MAENDELEO ISIMANI.


MATUKIO DAIMA MEDIA, ISIMANI

Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemsifu mgombea ubunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, kwa usimamizi makini wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu.

Akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa kampeni za Jimbo la Isimani, Dkt. Nchimbi alisema Lukuvi amekuwa ni msimamizi hodari wa fedha za serikali, hali ambayo imewezesha miradi mingi kukamilika kwa wakati.

 “Lukuvi ni kiongozi wa maendeleo, si tu kwa Isimani bali hata kitaifa amekuwa akishiriki katika vikao vya mipango miji, lakini bado amejali zaidi jimbo lake hii ni tabia nzuri ya kuwapigania wananchi wake hivyo, tumsaidie kwa kumpigia kura nyingi yeye, Rais na madiwani Oktoba 29 ili yale tuliyoyapanga yakamilike,” alisema huku akiwatania wananchi.

Dkt. Nchimbi alieleza kuwa kwa mujibu wa Ilani ya CCM ya miaka mitano ijayo, serikali imejipanga kuboresha huduma za kijamii katika Jimbo la Isimani, ikiwemo kupandisha hadhi hospitali ya wilaya, kujenga vituo vipya vya afya 7, zahanati 15, shule za msingi 12 na sekondari 8 pamoja na madarasa 395 kwa shule zilizopo.

Aliongeza kuwa miradi mikubwa ya maji imetekelezwa, ikiwemo bwawa la umwagiliaji, na mipango ipo kwa ujenzi wa visima virefu vitano na kukamilisha skimu za Ifunda, Ihemi na Tungamalenga. Aidha, alisema sekta ya kilimo ambayo huzalisha zaidi ya tani 49,000 kwa mwaka, imepewa kipaumbele kwa mipango ya ruzuku na ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji.

Kwa upande wake, Lukuvi alibainisha kuwa serikali inajenga mfereji mkubwa zaidi katika Tarafa ya Pawaga wenye thamani ya shilingi bilioni 56.9, pamoja na mfereji wa Magonzi wa shilingi milioni 33.8. Alisema mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa mpunga kufikia tani 100,000 kutoka tani 46,000 za sasa.

Pia, Lukuvi alishukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya 6, hospitali ya wilaya, chuo cha ufundi VETA na shule 15 za sekondari.

Naye Mratibu wa Kampeni za CCM Nyanda za Juu Kusini, Salim Abri, alisema Lukuvi ni kiongozi mzoefu anayejua changamoto za wananchi na ataendelea kuzitatua iwapo atarejea bungeni.

Kwa upande wake, kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa, alisema serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto kutoka 500 hadi 104 kwa mwaka, hatua inayodhihirisha dhamira ya chama hicho katika kuboresha maisha ya wananchi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI