Header Ads Widget

TANAPA KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI SHULE YA SEKONDARI MWANDETI WILAYANI ARUMERU MKOANI ARUSHA.


Na,Jusline Marco;Arusha

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) kupitia kitengo cha ujirani mwema  imeahidi kutoa kiasi cha shilingi Milioni 63 kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi wa maji katika shule ya sekondari Mwandeti ikiwa ni Moja ya uungaji mkono juhudi za serikali katika kuweka kipaumbele sekta ya elimu nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi,hifadhi za Taifa Tanapa Musa Nassoro Kuji wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maafali ya 19 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Mwandeti iliyopo Wilayani Arumeru, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya fedha na uhasibu TANAPA Moreen Mwaimale amewataka wadau wa elimu kuunga mkono juhudi hizo ili kuwafanya wanafunzi kuwa katika mazingira mazuri.

Ameongeza kwa kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu na kuboresha miundombinu ya shule ambapo amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wema wa Uhifadhi katika utunzaji wa mazingira kwa maslahi mapana ya nchi.

Awali akizungumza katika maafali hayo Mkuu wa shule hiyo Mwl.Lekera Sakey amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1986 wavulana 793 na wasichana1193 ambapo kati ya hao wanafunzi 498 wanatarajiwa kufanya mtihani wao wa Taifa mwanzo mwa mwezi Novemba mwaka huu.

Ameongeza kuwa shule hiyo imefanikiwa kuanzisha elimu ya sekondari ya juu mnamo mwaka 2016 kwa wasichana katika tahasusi tatu ambazo ni HKL, HGK na HGF huku maendeleo ya kitaaluma kwa kidato cha nne yakiwa yanapanda siku hadi siku na kufanikiwa kuondoka daraja 0 ambapo lengo kubwa ni kuondoka daraja la nne.

Mwl.Sakey ameeleza kuwa matarajio yao kama shule ni kuiweka shule kwenye shule tano bora kitaifa kwa kuendelea kupata daraja la kwanza kwa upande wa A - level ambapo tayari mikakati imefanywa na inaendelea kufanyika baina ya walimu pamoja na wanafunzi kuhakikisha kuwa matokeo yote yataendelea kuiheshimisha halmashauri ya Wilaya ya Arusha pamoja na Mkoa mzima.

Amesema pamoja na serikali kutekeleza miradi mingi shuleni hapo, mwaka 2024/25 shule ilipata fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa bweni la wasichana lililokuwa katika hatua ya msingi ambapo kwa sasa ujenzi huo umekamilika na bweni hilo linatumika, pia ilipokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu 6 ya choo ambayo nayo yamekamilika na yanatumika.

Kwa upande wao wahitimu katika risala yao ilisomwa mbele ya mgeni rasmi na Kelvin Seleman amesema pamoja na malengo waliyonayo ya kupata wastani wa juu katika ufaulu kwenye mtihani wa Taifa, wamefanikiwa kushiriki kwa kuchangia ujenzi wa ukuta unaozunguka eneo la mbele la shule hiyo,kushiriki ukarabati wa bweni la wavulana kwa msaada wa walimu.

Amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo pia shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa huduma ya maji yenye uhakika,uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi hususani somo la fizikia,baiolojia na kemia,uhaba wa vitabu vya kujisomea ,maktaba ndogo ukilinganisha na idadi ya wanafunzi hali inayosababisha wanafunzi wengine kushindwa kutumia maktaba kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI