MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA.Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendeleza mshikamano, upendo na kuheshimiana, huku kila mmoja akitumia haki zake bila kuathiri haki za wenzake.
RC Kheri alitoa wito huo alipotoa salamu za pole kwa familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini, marehemu Frank John Nyalusi, nyumbani kwake katika Mtaa wa Mawelewele, Kata ya Mwangata.
Amesema mshikamano ulioonyeshwa na wananchi wakati wa safari ya mwisho ya marehemu Nyalusi ni uthibitisho kuwa marehemu alikuwa mtu wa watu, mwenye kukubalika vyama vyote na dini zote kutokana na matendo yake mema.
“Kila aliyekubali kuzaliwa amekubali kufa. Kwa wakati na mazingira ambayo Mungu atayaruhusu, kila mmoja atapita njia hii ambayo mwenzetu Frank ametangulia. Jambo la msingi ni kujiandaa kwa matendo mema ya kumpendeza Mungu,” alisema RC Kheri.
Aliongeza kuwa Iringa imeendelea kuwa mfano wa ustaarabu na mshikamano, huku wananchi wake wakijulikana kwa ujasiri, uzalendo na heshima katika mchakato wa maendeleo.
“Nyalusi kwa nje alionekana mwana Chadema, lakini kwa ndani alikuwa mtu wa watu. Alikuwa mkweli, hakuficha jambo lililomkera na alitoa msaada mkubwa kwa viongozi kubaini kasoro na kuzitatua,” alisema.
Aidha, aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuendeleza mshikamano katika familia ya marehemu, hususan kusaidia watoto katika masuala ya msingi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti na Mratibu wa Kamati ya Mazishi, Jackson Mnyawami, alimshukuru RC Kheri kwa kufika kuifariji familia ya marehemu, akisema ni faraja kubwa kwa wananchi kupata kiongozi anayejali matatizo ya watu wake.
Mnyawami alisema Nyalusi alikuwa kiongozi shupavu, rafiki wa kila mtu na mchapa kazi.
“Msiba huu umetufundisha kuwa mshikamano ni nguzo muhimu, hususan wakati wa changamoto za afya na misiba,” alisema.
Alitangaza kuwa jumla ya shilingi milioni 10.876 zimekusanywa kama rambirambi kutoka kwa wanachama na wananchi mbalimbali.
Chadema pia ilitoa shukrani kwa Matukio Daima Media chini ya Mkurugenzi wake Francis Godwin, kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja tangu msiba ulipoanza hadi mazishi.
Naye Patrick Ole Sosopi alisema Nyalusi ameacha pengo kubwa kwa wananchi na wanachama wa Chadema.
“Aliishi maisha yaliyogusa kila mmoja, na alikuwa mfano wa kuigwa nawaomba Watanzania kuenzi mazuri aliyotuachia na kuendelea kuwafariji wanafamilia,” alisema.
Marehemu Frank John Nyalusi alifariki dunia usiku wa kuamkia Septemba 19 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini na ameacha mke pamoja na watoto wanne.
MWISHO
0 Comments