POLISI mkoani Kigoma imesema kuwa imeanza uchunguzi kuhusiana na madai ya baadhi ya viongozi na wagombea wa vyama vya siasa mkoani Kigoma kununua kadi za kupigia kura (viparata) za baadhi ya wapiga huku lengo la kufanya hivyo likiwa bado halifahamiki.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kigoma alisema kuwa uchunguzi huo unakuja kufuatia barua ya malalamiko iliyoandikwa na Mgombe ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini (ACT Wazalendo), Kiza Mayeye kufuatia kufanyika kwa vitendo hivyo katika jimbo lake.
Kamanda Makungu alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ni kosa kwa mtu yeyote kununua au kuchukua kadi hiyo ya kupiga kura kutoka kwa mtu mwingine ambapo alibainisha kuwa jambo hilo linaangukia kwenye makosa ya kuhujumu na kuvuruga uchaguzi.
Awali akiongea na waandishi wa habari Mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini kwa Chama Cha ACT Wazalendo, Kiza Mayeye alieleza kuwepo kwa vitendo vya kuandikisha kadi za wapiga kura kunakofanywa na moja ya chama cha siasa jambo ambalo anaeleza kuwa ni kinyume na taratibu za uchaguzi.
Mayeye alisema kuwa upo ushahidi wa watu waliokamatwa wakifanya vitendo hivyo na kufikishwa polisi huku wakijitetea kwamba wanaandika kadi hizo kwa ajili ya suala la kugawa mbolea, kuandika walengwa wa TASAF wakitumwa na mamlaka za kiserikali.
Mgombea huyo alisema kuwa jambo hilo limeenda mbali Zaidi kwa baadhi ya watoto kutumwa kuiba kadi hizo za kupigia kura za wazazi wao na kupewa fedha huku wazazi wakiwa hawajui vitambulisho vyao vimeenda wapi.
0 Comments