Na Matukio Daima Media, Iringa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limethibitisha kupatikana kwa Padri Jordan Kibiki wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mafinga, ambaye awali aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa Padri huyo hakutekwa bali alitoa taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatsApp, akidai kuwa ametekwa na kupelekwa Mbeya kwa gari aina ya Toyota Alphard nyeusi.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Padri Kibiki alikuwa anakabiliwa na madeni makubwa baada ya kukopa fedha kwa watu mbalimbali na kushindwa kuzirejesha.
Fedha hizo alizitumia kufanya biashara mtandaoni kupitia kampuni iitwayo eBEY. Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa uchunguzi unaendelea na mara ukikamilika, Padri huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kutoa taarifa za uongo na udanganyifu.
Mbali na tukio hilo, Jeshi la Polisi pia limefafanua kuhusu matukio mengine mawili yaliyotokea mkoani hapa.
kuwa Juni mwaka huu, Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano kwa tuhuma za utakatishaji wa fedha na udanganyifu kupitia mwavuli wa dini.
Miongoni mwao ni Yanick Mbombo Cele, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mchungaji wa Kanisa la Ebenezer Restoration Ministry for All Nations tawi la Iringa, pamoja na wenzake wanne.
Uchunguzi ulionesha kuwa Mchungaji Yanick alikuwa akitapeli waumini kwa madai ya kuwa na uwezo wa kufanya miujiza ya uponyaji.
Baada ya makubaliano ya kisheria (plea bargain), magari matatu aliyokuwa akimiliki yalitaifishwa na kulipa faini ya Shilingi milioni 200 kabla ya kuondolewa nchini.
Katika tukio la tatu, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Iringa mnamo Septemba 15, 2025, liliwakamata Mansour Ahmed na Japhet Masunga, wafanyabiashara wakazi wa Mkimbizi, wakiwa na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 2,995.74 na thamani ya Shilingi milioni 755.
Vifaa vya kuchakata na kuosha dhahabu pamoja na bajaji waliokuwa wakitumia pia vilikamatwa na kukabidhiwa kwa Afisa Madini wa Mkoa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Allan Bukumbi ametoa onyo kali kwa viongozi wa dini na wananchi kuepuka kujihusisha na vitendo vya udanganyifu na kinyume cha sheria vinavyoweza kuleta taharuki katika jamii. Pia amewataka wananchi kupata taarifa sahihi kutoka mamlaka husika badala ya kuamini kila kinachochapishwa mitandaoni.
0 Comments