Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua amesema kuwa kutolewa kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wajasiliamali kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kumekuwa na tija kubwa kubwa katika kutengeneza ajira kwa watu mbalimbali.
Dk.chuachua alisema hayo akikabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 555.6 kwa vikundi vya wajasiliamali zilizotolewa kupitia benki ya CRDB.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa Kutolewa kwa mikopo hiyo kumewafanya wajasiliamali kupanua na kuimarisha shughuli zao na kuweza kuajiri watu wengi zaidi hivyo kufanya shughuli zao kuwa na tija kwani wengi wao shughulizao zilidumaa kwa kukosa fedha za kutekeleza mambo ambayo yanazipa uhai biashara hizo ikiwemo masoko.
Chuachua alisema kuwa wataendelea kuisimamia halmashauri kuhakikisha mikopo Zaidi inatolewa kwa wajasiliamali kwani hilo ni agizo la Raisi kwa Halmashauri zote nchini hivyo wajibu wao kuzisimamia halmashauri kuhakikisha zinatekeleza agizo hilo.
Awali Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji, Jabiri Majira alisema kuwa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 555.6 imetolewa kwa vikundi 58 vya wajasiliamali kutoka makundi maalum ili kuwezesha wajasiliamali hao kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Majira alisema kuwa kutolewa kwa mikopo hiyo ni muendelezo wa halmashauri hiyo kutoa mikopo kwa makundi maalum ili kutekeleza agizo la Rais Samia la kutoa mikopo kwa makundi hayo kuwezesha kuimarisha shughuli zao za uchumi na biashara kuwa na tija na kwamba kwa mwaka huu pekee tayari inafanya kiasi cha shilingi Zaidi ya milioni 600 kuwa kimetolewa.
Akieleza kuhusu utoaji wa mikopo hiyo Afisa Ruzuku wa Benki ya CRDB Makao Makuu,Baraka Kayila alisema kuwa kupitia benki ya CRDB katika program yake ya imbeju CRDB inatoa mikopo kwa wajasiliamali kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri ili kutekeleza agizo la serikali la halmashauri kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.
Mwisho.







0 Comments