Header Ads Widget

MAELFU WAENDELEA KUJITOKEZA MIKUTANO YA HADHARA YA KAMPENI YA MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA VUNJO, ENOCK KOOLA


Na Ashrack Miraji Matukio Daima 

Kahe Mashariki, Vunjo Maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni ya mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Enock Koola, ambaye Jana  ameongoza mkutano mkubwa wa hadhara katika Kata ya Kahe Mashariki.

Mkutano huo wa kampeni, ambao ni wa kwanza rasmi kwa Mhe. Koola tangu kuanza kwa harakati za kuomba kura, umeonesha mvuto mkubwa kwa wananchi wa Vunjo, huku wengi wakijitokeza kuonesha ushirikiano na imani yao kwa mgombea huyo kijana na mwenye maono. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya kata na wilaya.

Katika hotuba yake, Mhe. Enock Koola alitumia jukwaa hilo kuwaomba wananchi wamchague yeye kama Mbunge wa Vunjo, lakini pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo nchini na hasa katika mkoa wa Kilimanjaro


“Nawaomba wananchi wa Kahe Mashariki na Vunjo kwa ujumla, tutumie fursa hii kuhakikisha tunampatia kura za kutosha Mhe. Rais Samia pamoja na madiwani wa CCM ili tuweze kuendelea kusukuma maendeleo kwa kasi zaidi,” alisema Koola huku akishangiliwa na wananchi.

Aidha, mkutano huo uliambatana na burudani mbalimbali na pia fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa mgombea, hali iliyowafanya wengi kujisikia kushirikishwa na kuthaminiwa. Kampeni za Mhe. Enock Koola zinatarajiwa kuendelea maeneo mengine ya jimbo hilo katika siku chache zijazo, huku matarajio yakiwa makubwa kwa ushindi wa kishindo kwa tiketi ya CCM.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI