Header Ads Widget

MABALOZI WA USALAMA BARABARANI, MAAFISA USAFIRISHAJI NA WAMILIKI WA VYOMBO VYA MOTO WAPEWA MAFUNZO YA BIMA.

 

Mabalozi wa usalama barabarani, Maafisa usafirishaji na Wamiliki wa vyombo vya moto Mkoani Mwanza wamepewa mafunzo ya bima na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika sekta ya usafirishaji.

Katibu wa Ubalozi wa Usalama Barabarani Subira Sabi, ameeleza kuwa wamepata mafunzo kuhusu namna taasisi za bima zinavyofanya kazi na jinsi abiria wanavyonufaika wanaposafiri kwa vyombo vilivyosajiliwa kisheria.


Sabi ameeleza kuwa mabasi yaendayo  Mikoani na daladala hukatia bima kila siti ya abiria, jambo ambalo wengi halikuwa hawalijua. Pia alieleza hasara zinazoweza kumpata abiria anapopanda magari binafsi ambayo hayajasajiliwa kisheria kwa ajili ya usafirishaji kwani ikitokea amepatwa na ajali hupoteza haki zake za msingi za kupewa fidia.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bima Kanda ya Ziwa, Oyuke Phostine, Alisema elimu hiyo waliyoitoa kwa maafisa usafirishaji na wamiliki wa vyombo vya moto ni kutokana na wao kuwa wadau muhimu wa sekta ya bima, huku lengo ikiwa ni kuwajengea uelewa wa namna bora ya kukata bima ili iweze  kuwalinda wateja wao, lakini pia na namna ya  kuwasilisha madai kwa kampuni za bima endapo majanga yatatokea.


Phostine alisema pamoja na mwamko wa bodaboda na bajaji katika kukata bima, bado kuna changamoto ya usimamizi kwani mara nyingi hukwepa ukaguzi wa askari wa barabarani. Alisisitiza kuwa kukwepa bima si jambo la hekima bali ni kujitafutia majanga, na iwapo ajali itatokea, fidia hupatikana kwa yule aliye na bima halali kwa mujibu wa sheria.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bajaji, Mansuli Ahmada, alisema kupitia elimu hiyo wameelezwa namna ya kuthibitisha bima kwenye mfumo wa mtandaoni na jinsi ya kufikisha malalamiko iwapo kampuni imeshindwa kutimiza majukumu yake.

Alisema bima ni msaada mkubwa kwani humuepusha mmiliki wa chombo cha moto na gharama kubwa endapo atapata ajali, tofauti na wale wasiokuwa na bima ambao hulazimika kulipa hasara kwa fedha zao.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI