NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
Makumbusho ya Muhula wa Zama za Mawe Isimila (Isimila Stone Age Site Museum) yaliyopo Mkoani Iringa nchini Tanzania yametangazwa kuwa mshindi miongoni mwa mawasilisho bora ya urithi na utafiti wa pamoja kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Makumbusho (ICOM 2025) unaofanyika Roma, Italia kuanzia tarehe 24-27 Septemba.
Hayo yamesemwa na Mhifadhi Mambo ya Kale Mkuu kutoka Kituo cha Nyumba ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Magomeni, Bi. Neema Mbwana ambaye anashiriki katika mkutano huo unaofanyika Roma Italia akiambatana na Bwana Benedict Jagadi Mhifadhi Msaidizi na Bi. Amina Salum, Mhifadhi Mwandamizi.
"Ushindi huu umepatikana baada ya andiko nililoandika kuhusu Makumbusho haya lililowasilishwa kwenye mashindano ya kitaaluma yajulikanayo kama ICOM na likachaguliwa miongoni mwa washindi" amesema Bi. Neema.
Aidha,amefafanua kuwa ushindi huo unaonesha thamani ya kipekee ya Makumbusho ya Isimila kama eneo lenye zana za mawe za zaidi ya miaka 300,000, nguzo za asili na historia inayounganisha mabara.
Amesema wasilisho lilijikita katika kuoonesha muunganiko na mfanano wa Isimila na Hifadhi ya Taifa Ruaha ambapo pia imejaliwa kuwa na nguzo za Asili ‘Magda Natural pillars’.
Vile vile, Tanzania kupitia TANAPA imeshiriki kikamilifu, ikiwasilisha maono ya kulinda urithi huu kupitia ushirikiano, uhifadhi endelevu na ushirikishwaji wa jamii.
Mkutano huo unatoa fursa ya kuyatangaza maeneo hayo kimataifa na kuvutia watafiti na wageni wengi kuja kutembelea vivutio hivyo.
MWISHO.
0 Comments