Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amefungua rasmi kikao kazi cha kuandaa Mpango Mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031, akisisitiza umuhimu wa kuwa na malengo na mwelekeo thabiti ili kuiwezesha wizara hiyo kufanikisha malengo yake kwa ufanisi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho kilichowakutanisha Wakuu wa Idara, Vitengo pamoja na Maafisa Bajeti wa wizara hiyo, leo Septemba 23, 2025, jijini Dodoma, Dkt. Abbas amesema kuwa kazi ya kuandaa mpango huo ni ya msingi kwa maendeleo ya wizara kwa kuwa utasaidia kuchambua mahitaji ya muda mrefu na maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuongeza ufanisi wa utendaji.
“Tunapozungumzia Mkakati (Strategic Plan), tunamaanisha mpango kazi wa muda mrefu. Nina imani mkakati huu utaweza kuchambua mahitaji ya muda mrefu ya Wizara ili tufanikishe malengo yetu,” amesema Dkt. Abbas.
Aidha, amewataka viongozi hao kuainisha fursa zilizopo katika sekta ya maliasili na utalii, akieleza kuwa kwa kuweka mikakati madhubuti, wizara inaweza kupata watalii wengi zaidi endapo mkakati huo utaainisha fursa hizo, zilizopo nchini Tanzania.
Pia, amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanatengeneza mpango mkakati unaotekelezeka kulingana na hali halisi ya sekta hiyo, ambao utajumuisha maeneo mbalimbali kama ya kijamii, Dira ya Taifa 2025–2050 pamoja na masuala mtambuka yanayogusa sekta ya maliasili na utalii hapa nchini .
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema uandaaji wa mpango mkakati huo ni muhimu, kwa kuwa taasisi nyingi duniani zinazofanikiwa hutegemea mikakati ya muda mrefu.
Amesisitiza kuwa licha ya Tanzania kuwa na vivutio vingi, kama idadi kubwa ya simba na maeneo ya kipekee ya utalii, mambo yote haya yanahitaji mpango mkakati madhubuti ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya utalii kwa ujumla
Naye, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo, Bw. Abdallah Mvungi, amesema kuwa kikao hicho kitakuwa cha siku mbili, na kitatumika kama ramani itakayoiwezesha wizara kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aliongeza kuwa kikao hicho pia kitajumuisha mafunzo ya vitendo yatakayosaidia makundi maalum kutambua masuala ya kibajeti kwa ufanisi zaidi.
0 Comments