Wanafunzi kutoka China katika vyuo vikuu vya Uingereza wanashinikizwa kuwapeleleza wanafunzi wenzao ili kujaribu kuzuia mjadala wa masuala ambayo ni nyeti kwa serikali ya China, ripoti mpya inafichua.
Taasisi ya fikra tunduizi ya UK-China Transparency (UKCT) inasema uchunguzi wake pia uliangazia ripoti za maafisa wa serikali ya China kuwaonya wahadhiri kuepuka kujadili mada fulani katika madarasa yao.
Inakuja siku chache baada ya sheria mpya kuanza kutekelezwa ya kuweka wajibu zaidi kwa vyuo vikuu kudumisha uhuru wa kitaaluma na uhuru wa kujieleza.
Ubalozi wa China mjini London uliita ripoti hiyo "isiyo na msingi na ya kipuuzi", na kuongeza kuwa China inaheshimu uhuru wa kujieleza nchini Uingereza na kwingineko.
Mdhibiti, Ofisi ya Wanafunzi (OfS), anasema uhuru wa kujieleza na uhuru wa kitaaluma ni "msingi" kwa elimu ya juu.
Sheria mpya, iliyoanza kutumika wiki iliyopita, inasema vyuo vikuu vinapaswa kufanya zaidi ili kukuza uhuru wa kitaaluma na uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na katika kesi ambapo taasisi zina makubaliano na nchi nyingine.
Vyuo vikuu vinaweza kutozwa faini ya mamilioni ikiwa vitashindwa kufanya hivyo, OfS imesema.
Hata hivyo, ripoti ya UKCT inasema baadhi ya vyuo vikuu vinasita kushughulikia suala la kuingiliwa na China kwa sababu ya kutegemea kwao fedha za ada za wanafunzi wa China.
Ripoti hiyo inadai kuwa baadhi ya wasomi wa China waliohusika katika tafiti nyeti wamenyimwa viza na serikali ya China, huku wengine wakisema wanafamilia waliorudi China walinyanyaswa au kutishiwa kwa sababu ya kazi zao nchini Uingereza.
Mada hizo nyeti zinaweza kuanzia sayansi na teknolojia hadi siasa na ubinadamu, ripoti hiyo inasema, kama vile ripoti hiyo inasema mfano wa mada hizo ni kama dhulma katika mkoa wa Xinjiang wa China, kuzuka kwa Covid au kuongezeka kwa kampuni za teknolojia za China.
Baadhi ya wanafunzi waliripoti vitisho kutoka kwa wanafunzi wengine au maafisa wengine wa China, na vile vile kutoka kwa wafanyakazi katika Taasisi za Confucius.
Hizi ni taasisi za ubia zinazofanya kazi katika vyuo vikuu kadhaa vya Uingereza, ili kuzileta pamoja taasisi za Uingereza na China, pamoja na wakala wa serikali ya China ambao hutoa ufadhili.
Hufundisha utamaduni na lugha ya Kichina kwenye vyuo vikuu vya Uingereza, lakini wamekosolewa kwa madai ya uhusiano na Chama cha Kikomunisti cha China.
0 Comments