Header Ads Widget

WABUNGE WA CCM WALIOANGUKA KURA ZA WAJUMBE


 Katika kile kinachoonekana kama mabadiliko ya upepo wa kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wabunge kadhaa waliokuwa wakitetea nafasi zao wamejikuta wakitemwa na wajumbe wa chama hicho katika kura za maoni zilizofanyika Agosti 4, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Ingawa matumaini yao ya kurejea kwenye kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu bado yapo mikononi mwa vikao vya juu vya CCM, uamuzi wa wajumbe unaonesha wazi kuwa baadhi ya majina makubwa huenda yakasalia kuwa historia.

Katika Jimbo la Vunjo, Dr. Charles Kimei ambaye amekuwa mbunge tangu 2020 ameangushwa na Enock Zadock Koola aliyeibuka mshindi kwa kura 1,999 dhidi ya Kimei aliyepata kura 861. Hii ni mara ya pili kwa Koola kushinda kura za maoni katika jimbo hilo, baada ya kufanya hivyo pia mwaka 2020, ingawa hakupitishwa.

Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amepoteza mbele ya Moris Makoi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi. Makoi alipata kura 2,148 huku Ndakidemi akijikusanyia kura 627 pekee.

Katika Jimbo la Iringa Mjini,Kyerwa, Mbunge Innocent Bilakwate ameangushwa na Khalid Nsekela aliyezoa kura 5,693 sawa na asilimia 71 huku Bilakwate akipata kura 1,567.

Katika Jimbom la Makambako, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Daniel Chongolo ameibuka mshindi wa kishindo kwa kura 6,151, na kumwacha mbali Deo Sanga (maarufu kama Jah People), aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15, ambaye alipata kura 470 tu sawa na asilimia 7.1. aliyekuwa mbunge Jesca Msambatavangu amejikuta nafasi ya nne kwa kura 408. Mshindi wa kura hizo ni Fadhil Ngajilo aliyepata kura 1,899, akifuatiwa na Wakili Moses (1,523) na Mchungaji Peter Msigwa (477).


Tabora Mjini, Shabani Mrutu ameongoza kwa kura 6,612, akimshinda kwa mbali aliyekuwa mbunge Emmanuel Mwakasaka aliyepata kura 228 pekee. Mwakasaka alizidiwa hata na wapinzani wengine kama Hawa Mwaifunga (326) na Kisamba Tambwe (395).

Geita Mjini, Constantine Kanyasu ambaye amehudumu kwa miaka 10, amepata kura 2,097 na kushindwa na Chacha Wambura aliyepata kura 2,145. Upendo Peneza alipata kura 1,272 na wengine waliambulia makumi ya kura.

Kwa Jimbo jipya la Katoro, aliyekuwa Mbunge wa Busanda, Tumaini Magesa, alihamia huko lakini akashika nafasi ya tatu kwa kura 1,265 nyuma ya Kija Ntemi (2,134) na Ester James (2,075).

Katika jimbo la Namtumbo, aliyekuwa Mbunge Vita Kawawa ameshindwa mbele ya Dkt. Juma Zuberi Homera, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Homera alipata kura 11,836 asilimia 92 huku Kawawa akipata kura 852.

Mtwara Mjini, Joel Arthur Nanauka ameibuka mshindi kwa kura 2,045 dhidi ya Hassan Mtenga Mbunge anayemaliza muda wake aliyepata kura 1,607.

Katika Jimbo la Lindi Mjini, Mbunge anayemaliza muda wake, Hamida Abdalla, ameangushwa na Mohamed Utali, aliyeibuka kidedea kwa kupata kura 1,474 kati ya kura 3,289 zilizopigwa. Hamida alipata kura 876 pekee, ishara ya wazi kuwa wajumbe wameamua kubadili mwelekeo wa uongozi katika eneo hilo.

Nyasa, hali haikuwa tofauti aliyekuwa Mbunge na Naibu Waziri wa zamani, Stella Manyanya, ameangushwa kwa kishindo na John Nchimbi, aliyepata kura 9,157 kati ya kura 10,695 zilizopigwa. Manyanya alipata kura 548 tu, matokeo ambayo ni pigo kubwa kwa mbunge huyo mkongwe aliyedumu kwa vipindi kadhaa ndani ya Bunge.

Katika Jimbo la Muleba Kaskazini, Adonis Bitegeko ameibuka mshindi kwenye kura za maoni za CCM kwa kumbwaga aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Mbunge wa muda mrefu, Dkt. Charles Mwijage. Ushindi huo umeweka historia mpya katika jimbo hilo, na kuongeza idadi ya vigogo waliotemwa kwenye mchakato wa ndani wa chama.

Haya ni baadhi ya majina ya wabunge walioshindwa kura za maoni. Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwenye vikao vya juu vya CCM, ambavyo vina mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha majina ya wagombea.

Hata hivyo, uamuzi wa wajumbe umetuma ujumbe mzito kwamba mabadiliko yanahitajika, na sura mpya zinaungwa mkono. Kwa waliokuwa wabunge waliokataliwa na wanachama wao, matumaini pekee yaliyobaki ni uamuzi wa huruma kutoka juu kama utakuwepo.

Je, vikao vya juu vitarejesha majina yaliyokataliwa na msingi wa chama, au vitaacha sauti ya wajumbe iwe sauti ya wananchi? Macho na masikio sasa yako Dodoma.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI