Mamia ya maafisa wa usalama wa Israel waliostaafu wakiwemo wakuu wa zamani wa mashirika ya kijasusi wamemtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuishinikiza serikali yao kukomesha vita huko Gaza.
"Ni uamuzi wetu wa kitaalamu kwamba Hamas haileti tishio tena la kimkakati kwa Israel," maafisa hao wa zamani waliandika katika barua ya wazi iliyosambazwa na vyombo vya habari siku ya Jumatatu.
"Mwanzoni vita hivi vilikuwa vita vya haki, vita vya kujihami, lakini tulipofikia malengo yote ya kijeshi, vita hivi vilikoma kuwa vita vya haki," anasema Ami Ayalon, mkurugenzi wa zamani wa shirika la ujasusi wa ndani Shin Bet.
Vita hivyo vinavyokaribia mwezi wa 23, "vinapelekea Taifa la Israel kupoteza usalama na utambulisho wake," Ayalon alionya katika video iliyotolewa kuandamana na barua hiyo.
Barua hiyo ikiwa imetiwa saini na watu 550, wakiwemo wakuu wa zamani wa Shin Bet na shirika la kijasusi la Mossad, inamtaka Trump "kumuelekeza" Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusitisha mapigano.
Israel ilianzisha operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza kujibu shambulio baya la Oktoba 7, 2023 lililofanywa na kundi la Hamas la Palestina. Katika wiki za hivi karibuni, Israel imekuwa chini ya shinikizo la kimataifa la kukubali kusitishwa kwa mapigano ambayo huenda mateka wa Israel walioachiliwa kutoka Gaza na mashirika ya Umoja wa Mataifa kusambaza misaada ya kibinadamu.
Lakini baadhi ya Israel, wakiwemo mawaziri katika serikali ya muungano ya Netanyahu, badala yake wanashinikiza majeshi ya Israel kusukuma mbele vita na Gaza kukaliwa kwa mabavu yote au kwa sehemu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, barua hiyo ilitiwa saini na wakuu watatu wa zamani wa Mossad: Tamir Pardo, Efraim Halevy na Danny Yatom. Wengine waliotia saini ni pamoja na wakuu watano wa zamani wa Shin Bet -- Αyalon pamoja na Nadav Argaman, Yoram Cohen, Yaakov Peri na Carmi Gilon -- na wakuu watatu wa zamani wa jeshi, akiwemo waziri mkuu wa zamani Ehud Barak, waziri wa zamani wa ulinzi Moshe Yaalon na Dan Halutz.
Barua hiyo inasema jeshi la Israel "limetimiza kwa muda mrefu malengo mawili ambayo yanaweza kufikiwa kwa nguvu: kuisambaratisha miundo ya kijeshi ya Hamas na utawala. Lakini, la tatu, na muhimu zaidi, linaweza kupatikana tu kupitia makubaliano: kuwaleta mateka wote nyumbani," iliongeza.
"Kuwafukuza wapiganaji wakuu waliosalia wa Hamas kunaweza kufanywa baadaye," barua hiyo ilisema. Katika barua hiyo, maafisa hao wa zamani wanamwambia Trump kwamba anaaminika na Waisraeli walio wengi na anaweza kuweka shinikizo kwa Netanyahu kumaliza vita na kuwarudisha mateka.
Baada ya kusitishwa kwa mapigano, waliotia saini wanasema, Trump anaweza kuutaka muungano wa kikanda kuunga mkono Mamlaka ya Palestina iliyofanyiwa mageuzi kuchukua mamlaka ya Gaza kama njia mbadala ya utawala wa Hamas.
0 Comments