Na Matukio Daima Media Kilolo
Mbunge wa zamani wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ritta Kabati, ameibuka mshindi wa kura za maoni katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Kilolo kwa kupata kura 4,565, na kuwaacha mbali wapinzani wake wote katika kinyang'anyiro hicho.
Katika mchakato huo uliofanyika kwa amani na utulivu, wagombea wengine waliokuwa wanawania nafasi hiyo walijikuta wakipitwa kwa idadi kubwa ya kura.
Novat Mfalamagoha alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,845, akifuatiwa na Nathan Mnyawami aliyepata kura 1,993, huku Festo Kipate akikusanya kura 1,352.
Wagombea wengine waliobahatika kupata kura chache zaidi ni Shamdi Nzogella aliyepata kura 1,111 na Mwalubadu Ngaga aliyepata kura 317.
Ushindi wa Kabati umetafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama uthibitisho wa kukubalika kwake kwa wananchi wa Kilolo na ndani ya chama chake kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka wakati akiwa mbunge wa viti maalum, hasa katika kuchangia maendeleo ya jamii na utetezi wa makundi ya wanawake, vijana na watoto.
0 Comments