Header Ads Widget

UDP YAAPA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA NA KUINUWA WANANCHI WANYONGE

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

MGOMBEA Urais wa Chama cha United Democratic Party (UDP), Saum Hussen Rashid, ametangaza dhamira yake ya kuongoza nchi kwa kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijinsia, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, pamoja na kuondoa sheria na sera kandamizi zinazowanyima haki wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni mwa maendeleo.


Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais, Saum  akiwa na mgombea mweza Juma Hamis Faki,ameeleza kuwa serikali ya UDP itakuwa ya wananchi wote na itaweka kipaumbele katika kupigania haki za binadamu, hasa haki za wanawake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

"Moja ya malengo makuu ya kampeni yangu ni kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma katika maendeleo. Tutapitia upya sera na sheria zote zinazokandamiza wanawake na kuhakikisha tunaweka mifumo inayowalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia," amesema Saum.

Aidha, ameipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa uwazi, haki na uhuru, akibainisha kuwa hadi sasa timu yake imeona mazingira yanayoruhusu wagombea kushiriki bila ubaguzi au upendeleo.

 Ametoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao kuhakikisha wanaendelea kuzingatia maadili ya uchaguzi ili kuepuka vikwazo visivyo vya lazima ambavyo vinaweza kuwanyima wagombea haki ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Katika kuwasilisha ajenda kuu za chama cha UDP,  Saum ametaja vipaumbele vyao kuwa ni kuboresha huduma za afya, kuinua ubora wa elimu, kuwekeza katika viwanda na biashara kwa lengo la kuongeza ajira, pamoja na kulinda mazingira na kudumisha hali ya amani na utulivu nchini.

"Tunataka kuona Tanzania mpya yenye usawa, haki, na maendeleo jumuishi. Tutawekeza kwenye huduma bora za jamii, hasa afya na elimu, lakini pia tutaweka mazingira rafiki ya biashara na viwanda ili kila Mtanzania anufaike," amesema mgombea huyo.


Amesisitiza kuwa wao ni chaguo mbadala kwa Watanzania, na kwamba wanakuja na ajenda ya mageuzi yatakayowagusa wananchi wa hali ya chini na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika safari ya maendeleo.

 Saum ameeleza kuwa chama cha UDP kimejipanga kushindana kwa hoja, sera na mikakati madhubuti ya kuijenga Tanzania mpya yenye usawa wa kijinsia, haki za kijamii, na ustawi wa kiuchumi kwa wote.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI