Header Ads Widget

POLISI WAUA WATATU KWA RISASI TUHUMA ZA UJAMBAZI

 

     

 Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Polisi mkoani Kigoma imewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi waliokuwa na lengo la  kufanya tukio la uhalifu wa kutumia silaha la kutaka kuteka magari  kwenye barabara kuu ya Kutoka Kasulu kuelekea Kibondo baada ya kufunga barabara kwa mawe makubwa.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu  alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi usiku katika eneo la Kumshindwi kijiji cha Kigendeka wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambapo watuhumiwa hao wanadaiwa kutaka kufanya tukio la uhalifu la kuteka magari.

Kamanda  Makungu alisema kuwa kabla ya kuuawa kwa watuhumiwa hao kulitokea majibizano ya risasi baina ya majambazi hao na polisi ambapo majambazi hao walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali ya wilaya Kibondo kwa matibabu ambapo walifariki dunia baadaye.


Pamoja na kuuawa kwa majambazi hao Kamanda Makungu alisema kuwa katika eneo la tukio walikuta bunduki moja aina ya AK 47 ikiwa na magazine moja yenye risasi 10, bunduki moja iliyotengenezwa kienyeji, panga moja na marungu matatu.

Awali Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa majambazi hao waliweka mawe makubwa barabarani kwa nia ya kuteka magari ambayo yangepita kwenye barabara hiyo ambapo polisi walipata taarifa na kufika eneo la tukio kabla hayajatokea madhara na kufanikiwa kuzima tukio hilo la utekaji.

kufuatia tukio hilo Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapowaona watu wenye mashaka kwenye maeneo yao au kuona watu wenye nia ya kutaka kufanya uhalifu.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI