Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewakumbusha wawekezaji kuhakikisha wanakuwa na cheti cha tathmini ya mazingira (EIA) kabla ya kufanya uwekezaji wowote
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Kati-Dodoma, Novatus Mushi, wakati akitoa elimu kwa umma kwenye maonyesho ya wakulima yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Dodoma.
Alisema sheria inawataka wawekezaji wote kuhakikisha wanakuwa na EIA na wale ambao wamekuwa wakikaidi wamekuwa wakitozwa faini kwa ukiukwaji huo wa sheria ya mazingira.
Alisema NEMC inatoa kipaumbele kutoa elimu kwa umma kabla ya kufanya ukaguzi wa kuwabaini watu wanaokiuka sheria ya mazingira kwenye maeneo mbalimbali nchini.
“Hapa kwenye banda letu tunatoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya mazingira na tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha kina uwekezaji unaofanywa unazingatia sheria na wale wanaokutwa wamekiuka sheria taratibu za sheria zinachukuliwa,” alisema
Alisema katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea NEMC inaelimisha umma kuhusu kuendesha kilimo, uvuvi na ufugaji unaozingatia misingi ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
“Maonesho haya ya mwaka 2025 yaliyobebwa na kaulimbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi” –ni ujumbe ambao NEMC wameutafsiri kwa vitendo kwa kuonesha kuwa maendeleo ya kweli katika sekta hizo hayawezi kufikiwa bila kulinda rasilimali asilia kama ardhi, maji, na misitu,” alisema.
Alisema kilimo hifadhi ndio njia sahihi ya kwenda mbele katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi na upungufu wa maji.
“Tunafundisha wakulima mbinu kama kutumia mboji, kulima kwa matuta, na kutumia mimea ili kupunguza mmomonyoko wa udongo na kupandisha tija bila kuharibu mazingira,” alisema.
Alisema kwa upande wa ufugaji, NEMC inahamasisha ufugaji wa kisasa usiochafua mazingira kwa njia ya kupunguza uchafuzi wa vyanzo vya maji na matumizi ya vyakula visivyotumia kemikali nyingi.
Aidha, alisema wanatoa elimu kuhusu matumizi bora ya majitaka kutoka mabwawa ya kufugia samaki, pamoja na ujenzi wa mabwawa rafiki kwa mazingira kwa ajili ya uvuvi wa kudumu ambapo wananchi wengi waliotembelea banda hilo wameonesha kufurahishwa na elimu wanayopata.
Alisema usimamizi thabiti wa mazingira ni sehemu muhimu ya mafanikio ya kilimo hifadhi, ufugaji endelevu na uvuvi salama – mambo ambayo yanahitaji uongozi makini na elimu kwa jamii nzima.
0 Comments