Header Ads Widget

KAZI ZA LUKUVI JIMBONI ZAMBEBA WANANCHI WA ISMANI: “WASEMA WANATIKI KWA LUKUVI ”

 

Na Matukio Daima Media, Iringa

Wananchi wa Jimbo la Ismani mkoani Iringa wameonesha wazi imani yao kwa aliyekuwa mbunge wao kwa miaka kadhaa, William Vangimembe Lukuvi, wakisema kuwa licha ya kuwepo kwa wagombea wengine waliopitishwa katika mchakato wa kura za maoni, bado chaguo lao linaelekea kwa Lukuvi kutokana na kazi kubwa alizozifanya akiwa mbunge.


Wakizungumza wakati wa hitimisho la kampeni za uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana, wapiga kura hao walisema kuwa wamemsikiliza kila mgombea aliyesimama mbele yao kuomba ridhaa, lakini kwa mtazamo wao, hoja na sera zilizowasilishwa na wagombea hao zimeshindwa kuwagusa moja kwa moja tofauti na historia ya utendaji kazi wa Lukuvi.

“Hatuwezi kusahau alichokifanya Lukuvi”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Idodi , Pawaga  ,Migori walikiri kuwa miaka yote ambayo Lukuvi amekuwa mbunge wa jimbo hilo, wameona mabadiliko makubwa katika sekta za afya, elimu, barabara na kilimo – hasa eneo la umwagiliaji katika bonde la mto Ruaha.


John Kalinga mkazi wa Mgama alisema kuwa ni rahisi mtu kuja na hotuba nzuri ya kisiasa lakini kutokuwa na dira ya kweli ya maendeleo. “Wagombea wengi walichofanya ni kulalamika, wengine kusema wamesahaulika lakini hawajasema wanataka kwenda kufanya nini. Sisi hapa Ismani hatuhitaji porojo, tunataka kazi kama zile za Lukuvi,” alisema Kalinga.


Obadia Sanga, mkazi wa Pawaga naye alisema kuwa Lukuvi hakuwahi kuwa mbunge wa maneno mengi bali wa vitendo, na kwamba kama kweli wagombea wapya wanataka nafasi hiyo, walipaswa kuonyesha mpango mbadala wa kimaendeleo, siyo kumshambulia aliyewatangulia.


Kiswaga alaumiwa kwa mwelekeo wa kampeni zake

Wananchi hao pia walihoji mwenendo wa kampeni za mgombea mwenzao Festo Kiswaga ambaye walimtaja kuwa alikuwa na nafasi nzuri ya kushindana lakini akaiharibu kwa kushambulia mtu badala ya kueleza mipango yake kwa wananchi.


“Badala ya kuja na sera, Kiswaga amekuja na shutuma. Anaonesha wazi ana kinyongo na Lukuvi. Hiyo siyo siasa tunayoitaka Ismani. Siasa ya maendeleo inataka uoneshe mipango yako, siyo kutilia shaka kazi ya mwingine tu,” alisema mama Sara Mgeni wa Kalenga.


Aidha, walishangazwa na kauli ya Kiswaga kuwa maendeleo ya Ismani yameletwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na madiwani bila kumtambua mbunge aliyesimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa karibu. “Kumtaja Rais na madiwani bila kumtaja mbunge ni sawa na kusema mafiga mawili yanaweza kupika. Hii ni chuki binafsi ambayo haileti mshiko kwa wananchi,” aliongeza mama huyo.


Wananchi wataja mafanikio ya Lukuvi

Wananchi hao waliendelea kufafanua mafanikio makubwa ambayo wameyaona katika kipindi chote cha utawala wa Lukuvi. Walitaja mradi wa barabara ya lami kutoka Samora mjini Iringa hadi Ruaha National Park, miradi ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, pamoja na upatikanaji wa dawa na watumishi.


Katika sekta ya elimu, waliipongeza serikali lakini wakasema juhudi za Lukuvi za kusimamia ujenzi wa madarasa, mabweni na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia zimekuwa chachu ya maendeleo ya elimu katika kata nyingi za jimbo hilo.


Katika hotuba yake ya kufunga kampeni, Lukuvi aliorodhesha baadhi ya miradi ambayo imekamilika na mingine inayoendelea, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika bonde la Pawaga ambalo limekuwa tegemeo kubwa la kilimo kwa wakazi wa maeneo hayo na sehemu nyingine za Iringa.


Aliwataka wapiga kura kuangalia historia ya kazi na si maneno. “Kampeni ya matusi na lawama haitujengi. Tunahitaji watu wa kazi, siyo watu wa malalamiko. Niliwahi kuwaambia wananchi wa Ismani kuwa sitakuwa mbunge wa mikutano mingi bali wa kazi. Leo mmeona, kazi zile zipo,” alisema Lukuvi.


Wito kwa CCM

Baadhi ya wazee na viongozi wa mitaa walitoa wito kwa Chama Cha Mapinduzi kutenda haki katika mchakato wa kura za maoni kwa kuzingatia rekodi ya utendaji wa wagombea. “Lukuvi si jina tu, ni historia ya kazi. Kura zetu tunampa yeye kwa sababu tunajua atatusaidia zaidi ya maneno,” alisema mzee Rashid Juma  wa kijiji cha Mboliboli.


Kwa ujumla, sauti za wananchi wa Ismani zinaonekana kuonyesha shukrani na matumaini yao ya kuendelea kupata maendeleo kupitia kiongozi ambaye wamekuwa naye kwa muda mrefu. Wakati kura za maoni zikiwa zimekaribia kupigwa, ujumbe wao ni mmoja: “Tumesikiliza wote, lakini bado tunamtiki Lukuvi.”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI