Israel imekataa vikali ukosoaji kutoka kwa viongozi wa dunia baada ya baraza lake la mawaziri la usalama kuidhinisha mpango wa kuudhibiti mji wa Gaza.
Waziri wa Ulinzi Israel Katz alisema nchi ambazo ziliilaani Israel na kutishia vikwazo "hazitadhoofisha azimio letu".
"Adui zetu watatukuta kama ngumi moja kali, iliyoungana ambayo itawapiga kwa nguvu kubwa," aliongeza.
Uamuzi wa Israel wa kupanua vita vyake huko Gaza ulizusha shutuma kutoka kwa Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Canada, na kusababisha Ujerumani kusitisha mauzo ya kijeshi kwa Israel.
Mpango huo ulioidhinishwa na baraza la mawaziri la usalama la Israel, unaorodhesha "kanuni" tano za kumaliza vita: kuwapokonya silaha Hamas, kuwarudisha mateka wote, kuuondoa kijeshi Ukanda wa Gaza, kuchukua udhibiti wa usalama wa eneo hilo, na kuanzisha "utawala mbadala wa kiraia ambao sio Hamas wala Utawala wa Palestina".
Ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zinasema mpango huo awali unalenga kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Gaza, kuwahamisha wakazi wake wanaokadiriwa kufikia milioni moja.
Vikosi pia vitachukua udhibiti wa kambi za wakimbizi katikati mwa Gaza na maeneo ambayo mateka wanafikiriwa kushikiliwa.
Shambulio la pili litafuata wiki kadhaa baadaye sambamba na kuongezwa kwa misaada ya kibinadamu, vyombo vya habari vinasema.
Hatua ya kuzidisha mzozo huo imepata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya watu ndani ya Israel, wakiwemo maafisa wa kijeshi na familia za mateka wanaozuiliwa huko Gaza.
Hamas imesema mpango wa kuukalia mji wa Gaza "unajumuisha uhalifu mpya wa kivita" na "utaigharimu [Israeli] kwa kiasi kikubwa".
0 Comments