Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimepiga hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kupitisha rasmi ilani yake ya uchaguzi pamoja na kuwateua wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa nchi.
Katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichofanyika leo Agasti 14,2025 Jijini Dodoma chama kimemtangaza Haji Ambar Khamis kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Dkt,Averline Munisi akiteuliwa kuwa mgombea mwenza. Kwa upande wa Zanzibar, nafasi ya urais itagombewa na Laila Rajab Khamis.
Uongozi wa chama hicho umesema kuwa uteuzi huo umefanywa kwa maridhiano na mashauriano ya kina ndani ya chama ambapo majina hayo yako tayari kuwasilishwa kwa wananchi kupitia kampeni zitakazozingatia maadili, haki, na utu wa Mtanzania.
Uongozi huo wa chama umesisitiza kuwa lengo la NCCR Mageuzi si kuiondoa tu Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani, bali kuendeleza mafanikio yaliyopo kwa misingi ya haki, usawa na maendeleo jumuishi.
Chama pia kimethibitisha kuwa kimesimamisha wagombea ubunge katika majimbo yote 162 nchini.
Ilani ya uchaguzi ya NCCR Mageuzi kwa mwaka 2025 imeweka vipaumbele katika maeneo muhimu ya maisha ya wananchi ikiwemo sekta ya afya, usawa wa kijinsia, maendeleo ya makundi maalum, mifugo, madini, maliasili na utalii, usalama wa taifa, pamoja na kurejesha maadili ya kitaifa.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahongo, aliyewakilisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, aliipongeza NCCR Mageuzi kwa kuonyesha utayari wa kushiriki uchaguzi na kutumia haki yao ya kikatiba.
Amesema kuwa uteuzi wa wagombea wa chama hicho umefanyika kwa uwazi na kwamba wagombea walioteuliwa ni watu makini na wenye maono.
Aidha, amewataka wanachama na viongozi wa chama kuendesha kampeni kwa utulivu na kwa kuzingatia sheria, akibainisha kuwa ni hiari kwa chama kushiriki au kutoshiriki uchaguzi kwa mujibu wa Katiba.
Chama hicho kimeeleza dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi bila kutegemea ruzuku ya serikali, bali kupitia michango ya wanachama na wapenzi wake, hali inayoonyesha dhamira ya kweli ya kujenga siasa safi na ya uwajibikaji nchini.
0 Comments