Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimepiga hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kupitisha rasmi ilani yake ya uchaguzi pamoja na kuwateua wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa nchi.
Katika kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichofanyika leo Agasti 14,2025 Jijini Dodoma chama kimemtangaza Haji Ambar Khamis kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Evans Munisi akiteuliwa kuwa mgombea mwenza. Kwa upande wa Zanzibar, nafasi ya urais itagombewa na Laila Rajab Khamis.
Uongozi wa chama hicho umesema kuwa uteuzi huo umefanywa kwa maridhiano na mashauriano ya kina ndani ya chama ambapo majina hayo yako tayari kuwasilishwa kwa wananchi kupitia kampeni zitakazozingatia maadili, haki, na utu wa Mtanzania.
Uongozi huo wa chama umesisitiza kuwa lengo la NCCR Mageuzi si kuiondoa tu Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani, bali kuendeleza mafanikio yaliyopo kwa misingi ya haki, usawa na maendeleo jumuishi.
Chama pia kimethibitisha kuwa kimesimamisha wagombea ubunge katika majimbo yote 162 nchini.
0 Comments