Na Fatma Ally Matukio DaimaApp
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa nchini kujiepusha na lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa taifa la Tanzania hasa kuelekea uchaguzi Mkuu.
Wito huo ameutoa jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa ambapo amesisitiza kuwa vyama vya siasa vina wajibu wa kuendeleza misingi ya amani na mshikamano wa taifa.
Amesema kuwa, viongozi wa vyama vya siasa nchini ni vyema kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinafanyika kwa kistaarabu, bila kutumia lugha za matusi, kashfa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha tunu ya amani Taifa iliyopo.
"Nendeni mkafanye kampeni za kistaarabu mkiwanadi wagombea wenu, kuweni na lugha nzuri za kuzungumza, epukeni matusi, lugha za kashfa, kwani amani ya taifa hili ni muhimu kuliko chochote"mesema Jaji Mutungi.
Ameongeza kuwa, amani na mshikamano ni urithi ulioachwa na waasisi wa taifa, hivyo viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi.
"Kumbukeni kuna maisha baada ya uchaguzi, Uchaguzi si mwisho wa siasa wala maendeleo. Turithishe amani hii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo," amesema Jaji Mitungi.
Sambamba na hayo amewasihi , viongozi kutokubabaishwa na upotoshaji unaoweza kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii na makundi mengine katika jamii akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa taarifa zinazoleta taharuki wawe nazo makini.
"Mtaambiwa uchaguzi haupo, msikate tamaa. Uchaguzi upo, na jambo kubwa zaidi ni kuhakikisha tunaingia kwenye uchaguzi huru na wa haki kwani ninyi ndio wakala wa kwanza wa kuhakikisha hilo linatekelezeka," amehimiza.
Kwa upande wake, Mwasilishaji Kuhusu Sheria Wakili Edmumdi Mgasha amebainisha kuwa Kifungu cha kanuni za Uchaguzi 6(,1)(2) kinamtaka Msajili kuweka pingamizi dhidi ya Mgombea aliyeshindwa kuweka Wazi kiasi cha vyanzo vya gharama za Uchaguzi ndani ya siku 14 baada ya uteuzi.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya Siasa Juma Khatib amewataka viongozi na watendaji wa vyama vya Siasa kuzingatia kwa makini masharti ya sheria ya gharama za uchaguzi ili kuepusha dosari na kasoro katika uchaguzi mkuu wa Octoba 2025.
Amesema kuwa, historia inaonesha baadhi ya vyama vya Siasa na wagombea walikua na uwelewa mdogo walipotakiwa kuwasilishwa taarifa za gharama za uchaguzi jambo ambalo limesababisha dosari kubwa ndani ya uchaguzi.
"Sheria hii ilipokuja mwaka 2010 watu wengi hawakuwa na uwelewa wengine walijaza gharama za uchaguzi hewa wakidhani baada ya uchaguzi wanarejeshewa fedha baada ya uchaguzi, walitengeneza risiti za kughushi, kumbe haipo hivyo, leo tutapata elimu ya kutosha"amesema Khatib.
Aidha, amewataka viongozi hao kuyachukua mafunzo hayo kwa umakini mkubwa sana ili kuepusha migogoro hasa kuelekea kipindi hiki Cha uchaguzi, zoezi hili liendeshwe kwa uwazi na uadilifu.
0 Comments