Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
MGOMBEA Urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, ameanza rasmi safari yake ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini kwa kuchukua fomu ya kugombea katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na kutangaza kuanza kutafuta wadhamini katika kijiji alichozaliwa Mwandoya, kilichopo Jimbo la Kisesa, Mkoa wa Simiyu.
Akiongwa na waandishi leo Jijini Agosti 15 ,2025 Dodoma huku akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Fatma Abdulhabib Fejej, Mpina amesema uamuzi wa kuanzia nyumbani una maana kubwa kwake, kwani ni ishara ya kurudi kwenye mizizi na kutafuta ridhaa ya wananchi walioanza naye safari ya maisha.
“Nilipozaliwa ndipo ninapoanza kutafuta dhamana ya kuongoza taifa hili ni jambo la heshima na moyo wa shukrani kwa jamii yangu,” amesema Mpina mbele ya wanahabari.
Mpina ametoa wito kwa wananchi, hususan vijana, kujitokeza kwa wingi kuwa sehemu ya mchakato wa kidemokrasia kwa kuwadhamini yeye na chama chake. Ameeleza kuwa zoezi la kudhamini litaendelea katika mikoa mingine baada ya Simiyu.
“Niwaombe vijana wajitokeze kwa wingi ili tupate sifa, na hawatafuata mambo ya vyama bali maslahi ya taifa,” aliongeza.
Amesisitiza kuwa vipaumbele vya ACT Wazalendo vitatangazwa rasmi mara baada ya mchakato wa upatikanaji wa wadhamini kukamilika.
0 Comments