Header Ads Widget

MGOMBEA URAIS WA NCCR MAGEUZI AAHIDI KUWEKEZA KWA WINGI KATIKA SEKTA YA AFYA

 


Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma

MGOMBEA  Urais wa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis, ameweka bayana kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ni kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii, sekta ambazo amesema zimekuwa dhaifu kwa muda mrefu.

Akizungumza leo Agosti 15, 2025, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), akiwa na mgombea mwenza wake Dkt. Evaline Munisi, Khamis amesema chama chake kinalenga kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika eneo la rasilimali watu na vitu, ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote.


"Maendeleo ya watu hayawezekani kama afya na ustawi wa jamii vimedhoofika kama ilivyo sasa,"Amesema Khamis.

Ameeleza kuwa hali ya sasa katika sekta ya afya si ya kuridhisha, akitolea mfano wa watu wengi kukosa matibabu kutokana na gharama kubwa na uhaba wa vifaa na dawa katika hospitali mbalimbali nchini.

"Tumeona katika miaka ya hivi karibuni, watu wanakosa huduma ya afya katika hospitali zetu. Wengi wa ndugu, jamaa na marafiki zetu wamepoteza maisha kwa sababu hawakuweza kumudu gharama za matibabu," amesisitiza mgombea huyo.


Kwa mujibu wa Khamis, amesema chama cha NCCR Mageuzi kinaamini kuwa huduma bora za afya ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania na si suala la anasa au upendeleo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI