Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff atazuru Gaza siku ya Ijumaa kukagua maeneo ya usambazaji wa chakula, Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amethibitisha.
Leavitt alisema Witkoff atazuru eneo hilo pamoja na Balozi wa Marekani nchini Israel Mike Huckabee na "kufikia mpango wa kuwasilisha chakula zaidi na kukutana na wakazi wa Gaza ili kusikia moja kwa moja kuhusu hali hii mbaya akiwa huko".
Witkoff, ambaye yuko ziarani nchini Israel, pia alikuwa na mkutano "wenye tija" na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katibu wa habari aliongeza.
Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema watu 111 wameuawa, 91 kati yao walipokuwa wakitafuta msaada, saa 24 kabla ya Alhamisi adhuhuri.
Mkurugenzi wa hospitali aliambia BBC kuwa zaidi ya Wapalestina 50 waliuawa na wengine 400 kujeruhiwa walipokuwa wakisubiri chakula karibu na kivuko kaskazini mwa Gaza siku ya Jumatano.
Picha zilionyesha majeruhi karibu na kivuko cha Zikim wakichukuliwa kwa mikokoteni kupelekwa hospitali ya al-Shifa katika Jiji la Gaza.
0 Comments