Header Ads Widget

HALI NGUMU WAKIMBIZI WA DRC NCHINI

 

Baadhi ya wakimbizi wa DRC wanaohifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma
Naibu Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania James Ole Millya akizungumza katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya kasulu mkoani Kigoma
Waziri wa nchi Wizara ya masuala ya jamii,hatua za kibinadamu na Mshikamano wa DRC, Eve Bazaiba Masudi akizungumza na wakimbizi wa DRC wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma

Apoline Masumbuko Mkimbizi wa DRC katika kambi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma

 Na Fadhili Abdallah,Kigoma

HALI ngumu inawakabili wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kufuatia kupunguzwa kwa asilimia 50 ya huduma za kibinadamu hali inayofanya wakimbizi hao kuomba kurudishwa nchini kwao.

 Akitoa taarifa kwa Ujumbe wa mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Tanzania waliotembelea kambi hiyo na kuzungumza na wakimbizi hao Kaimu Mkuu wa kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Samuel Kuyi alisema kuwa huduma nyingine za kibinadamu kambi hapo zimepunguzwa.

Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na huduma ya mgao wa chakula ambapo kwa sasa asilimia 65 ya chakula inatolewa kulimganisha na taratibu za kimataifa, huduma za afya ambapo kwa sasa vituo vyote vya afya vimefungwa na kubaki kituo kimoja huku huduma za rufaa kwenda hospitali ya mkoa au kanda Bugando zimeondolewa.

Kuyi alisema kuwa pia taratibu za wakimbizi wa DRC kwenda nchi ya tatu Marekani,Canada na Ulaya zimezuiwa na hata taratibu za masomo kwa wakimbizi hao kwa sasa zimesimama baada ya mashirika yanayoshughulikia masuala ya elimu kufungwa hivyo wakimbizi hao wapo kambini hapo bila huduma zozote za elimu.

Kutokana na hali hiyo Wakimbizi wa DRC waliopo kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma akiwemo Apoline Masumbuko wameiomba serikali ya Tanzania, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Shirika la Umoja wa Matifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) kuwarudisha nchini kwao kutokana na hali ngumu ya maisha na upatikanaji duni wa huduma za kibinadamu katika kambi hiyo

Akizungumza kambini hapo Naibu Waziri wa Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki,James Ole Millya alisema kuwa pamoja na wakimbizi hao kuomba kurejea nchini mwao  hakuna mkimbizi wa DRC atalazimishwa kurudi nchini mwao bali suala la usalama na utu wa wakimbizi hao utazingatiwa kama ilivyo kwa wakimbizi wa Burundi ambao kwa sasa wanasaidiwa kurudi nchini kwao kwa hiari.

Kwa upande wake  Waziri wa nchii Wizara ya masuala ya jamii,hatua za kibinadamu na Mshikamano wa DRC, Eve Bazaiba Masudi bado maeneo mengi wanayotoka wakimbizi hao hayana Amani na hivyo siyo rahisi kuwarudisha huko na kwamba wanaangalia namna ya kuwatafutia maeneo yenye Amani wakimbizi wanaotaka kurejea Congo kwa sasa.

Naye   Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, Barbara Dotse alisema kuwa shirika hilo linaendelea kutafuta fedha ili huduma za kibinadamu kwa wakimbizi hao wa DRC ziweze kurejea kawaida huku wakitafuta suluhisho la kudumu la wakimbizi hao kurejea nchini mwao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI