Na Mwandishi Wetu
SIKU chache baada ya Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kuifuta kesi ya Kikatiba ya Kupinga uteuzi wa Dk. Samia Suluhu Hassan kugombea urais Oktoba 29 mwaka huu mmoja wa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ameibuka na kutaka kesi hiyo iwe fundisho kwa wana CCM wengine.
Akizungumza mjini Dodoma leo, mgongwe wa siasa nchini, Khamis Mgeja alisema binafsi ameridhishwa na hukumu hiyo ambayo inatoa somo na fundisho kwa akina Polepole (Humphrey) na kundi lake pamoja na wanachama wote wa CCM kuiheshimu Katiba na Kanuni za ihama hicho walizojiwekea.
Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation yenye makao yake wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, alisema kesi hiyo iliyofunguliwa na Dk. Godfrey Malisa ililenga kutaka kuleta mtafaruku ndani ya CCM na kutaka kuuaminisha umma kwamba viongozi wa chama hicho ni mbumbumbu.
“Binafsi nimeridhishwa kabisa na kitendo cha Mahakama Kuu iliyoketi chini ya Jopo la Majaji watatu kuifuta kesi hii, naamini imetenda hki. Nilimshangaa ndugu yangu Malisa baada ya kumsikia amekimbilia Mahakamani kupinga uteuzi wa Dk. Samia Suluhu Hassan kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu,”
“Nilijiuliza sijui ndugu yetu huyu mpaka kufikia kuchukua maamuzi hayo, ambayo mimi nayaita “maamuzi mfu” hakusoma vizuri vifungu vya Katiba ya chama chetu ya mwaka 1977 Ibara ya 100 kifungu kidogo cha (2) inaeleza wazi mamlaka ya mkutano mkuu wa CCM, sasa Malisa alifikiri Mahakama pia haitakiona kifungu hicho?,” alihoji Mgeja.
Ibara hiyo ya 100 kifungu kidogo cha (2) kinasomeka; nanukuu; “…..Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa utakuwa ndicho Kikao Kikuu cha CCM kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka ya mwisho,” mwisho wa kunukuu.
Mgeja alisema kwa uelewa wake yeye ni kwamba Mkutano Mkuu wa Taifa unaweza kufanya jambo lolote kwa maslahi ya chama na likawa halali kwa kuzingatia kifungu hicho cha Katiba na ndiyo maana pendekezo la awali ya kutaka Dk. Samia ateuliwe kuwa mgombea lilielekezwa kufuata utaratibu.
Hivyo ilibidi mchakato wa uteuzi wa wagombea hao wa CCM uchakatwe kwanza kuanzia chini kwenye Sekretarieti ya CCM Taifa, kisha Kamati Kuu baadae kufikishwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo nayo ilipeleka agenda hiyo kwenye Mkutano Mkuu na wajumbe kwa kauli moja walipitisha na hivyo uteuzi huo kuwa halali kabisa.
Aliendelea kueleza kuwa kutokana na hukumu hiyo ni vyema sasa wanachama wa CCM wote wakajiwekea utamaduni wa kusoma Katiba ya chama na kanuni zake ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza kwa watu kutafsiri vibaya maamuzi yoyote yanayotolewa na vikao vya ngazi za juu.
Alisema iwapo kila mwanachama wa CCM ataielewa vizuri Katiba ya CCM pamoja na kanuni zake anaamini hapatakuwepo na mitafaruku ambayo katika siku za hivi imekuwa ikijitokeza hali ambayo imesababisha baadhi ya watu wasiokitakia mema chama hicho kudai kuwa ndani ya CCM hivi sasa kuna mpasuko mkubwa.
Alisema haoni kama ndani ya CCM kuna mpasuko au uvunjifu wowote wa Katiba kama inavyodaiwa na kupotoshwa na watu wachache wenye uroho wa kutaka kupata madaraka pasipo kufuata utaratibu sahihi wa ndani ya chama kama inavyotokea kwa akina Malisa pamoja na mwenzake Humphrey Polepole.
“Niwaombe wana CCM wenzagu tushikamane hasa katika kipindi hiki cha ulimwengu wa utandawazi, tusipokuwa makini tunaweza kujikuta tunaparuana wenyewe kwa wenyewe kwa mambo ambayo hayapo bali yanazalishwa na kusambazwa na wenzetu wenye maoni “mfu” kwa lengo la kutaka kuichafua CCM,”
“Kama ilivyoelezwa na Mahakama, malalamiko ya ndugu yetu Malisa, yalipaswa kufuata utaratibu ambao chama chenyewe kimejiwekea, yaani kuandika barua rasmi kwenye kwenye vikao husika ya kupinga jambo lolote ambalo mwana CCM anaamini limekiukwa kwa mujibu wa Katiba badala ya kukimbilia mahamani kujidhalilisha,” alieleza.
Kwa upande mwingine Mgeja ameipongeza CCM chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na viongozi wenzake wote wa kitaifa ambao pamoja na Malisa kukimbilia Mahakamani wao hawakutetereka wala kuyumbishwa na maamuzi hayo.
Alisema hatua hiyo imeonesha wazi ukomavu wao ndani ya chama na kwamba kila mwana CCM mwenye mapenzi ya dhati na chama chake anapaswa kujifunza kutoka kwa viongozi hao ambao misimamo yao imara imeendelea kukifanya Chama cha Mapinduzi kuimarika zaidi hapa nchini.
“Nafikiri baada ya hukumu hiyo kutolewa, ilikuwa ni vyema kwa ndugu yetu Malisa kushituka na kukaa chini ajitafakari kwa kina na achukue maamuzi magumu ya kuwaomba msamaha viongozi wetu wa CCM Taifa na wana CCM kwa ujumla kutokana na kitendo alichokifanya na kuomba radhi ili asamehewe,”
“Mtu muungwana anapobaini ameteleza, basi hatua yake ya kwanza ni kujisafisha na kukiri kukosea na kisha kuwaomba radhi wenzake, naamini hakuna ambaye angekataa kumsamehe Malisa, naomba nimfikishie ushauri wangu hebu akubali kushindwa, na awaombe radhi wana CCM, naamini watamsamehe na kubaki akiwa mwanachama mtiifu ndani ya chama chake,” alieleza Mgeja.
Hivi karibuni mara baada ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa katika kikao chake cha Januari 19, 2025 kuwateua Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM na Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza, Malisa aliibuka na kupinga maamuzi hayo kwa madai katiba ya CCM imevunjwa.
Baada ya kuona pingamizi lake halikuwa na mshiko kwa viongozi wa CCM na wana CCM kwa ujumla ndipo alipoamua kukimbilia Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kuweka pingamizi na kutaka uteuzi wa Dk. Samia na Dk. Nchimbi utenguliwe na mchakato mzima wa kuwapata wagombea wa CCM uanze upya
0 Comments