Header Ads Widget

M23 YAITUHUMU SERIKALI KWA KUTUMIA MAMLUKI WA KIGENI KATIKA MASHAMBULIZI YANAYOENDELEA


 Wanamgambo wa M23 wameituhumu serikali ya DR Congo kwa kutumia “mamluki wa kigeni” katika mashambulizi ya Jumapili, ambayo wanadai yalilenga maeneo yanayokaliwa na jamii ya Kadasomwa pamoja na viunga vyake, katika eneo la Kalehe, mkoani Kivu Kusini.

Hata hivyo, jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) halijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo za M23.

Shirika la BBC liliwasiliana na msemaji wa jeshi kuhusiana na madai hayo ya matumizi ya mamluki, lakini bado hajatoa majibu.

Ripoti za mapigano kati ya pande hizo mbili ziliripotiwa siku ya Jumamosi na Jumapili katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kivu Kusini, ambapo mashuhuda mbalimbali wamedokeza kuwa mapigano hayo yamesababisha wakazi wengi kukimbia makazi yao.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa kundi la AFC/M23, Lawrence Kanyuka, alisema kuwa mashambulizi ya Jumapili huko Kadasomwa “yamesababisha vifo vya watu wengi” na “kuwaacha maelfu bila makazi” kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

Kanyuka aliongeza kuwa hapo awali, serikali iliwahi kutumia mamluki kutoka barani Ulaya, ambao waliruhusiwa kupitia Rwanda kurejea makwao baada ya M23 kuteka jiji la Goma.

Sasa, anadai kuwa mamluki waliotumika safari hii, ambao pia anawashutumu kwa kuhusika na mauaji, “hawatarudi kwa amani”.

Wakati huohuo, jeshi la Rwanda nalo linatuhumiwa kuisaidia M23, tuhuma ambazo serikali ya Rwanda imekanusha vikali.

Mapigano makali pia yalishuhudiwa siku ya Jumamosi katika eneo la Mwenga, mkoani Kivu Kusini, katika eneo la Efpo, na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa ripoti ya Radio RFI.

Inaripotiwa kuwa mapigano hayo pia yalipelekea kundi la M23 kuteka eneo la milimani la Lubumba, takriban kilomita 80 kutoka jiji la Uvira.

Pierre Mheshera, afisa wa serikali za mitaa katika jiji la Uvira, ameieleza BBC kuwa mapigano ya Jumamosi yamesababisha wakazi wengi “kuhama maeneo ya Lubumba na Kadjoka na kuelekea Uvira.”

Mheshera amethibitisha kuwa kwa mujibu wa taarifa walizonazo, M23 kwa sasa inalitawala eneo la Lubumba.

Taarifa hizi pia zimethibitishwa na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani nchini DRC.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa serikali wala kwa kundi la M23 kuhusu madai hayo.

Mwezi uliopita, pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika Doha, Qatar.

Mazungumzo hayo yalilenga kufikia mkataba wa amani ifikapo tarehe 18 mwezi huu, lakini malengo hayo hayakufikiwa.

Hata hivyo, pande zote mbili kwa sasa zimeendelea na mazungumzo mjini Doha.

Wakati mazungumzo yakiendelea, pande zote mbili zimeendelea kushutumiana kwa kuanzisha mashambulizi ya hapa na pale ambayo yameripotiwa katika mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI