Kikundi cha wanamgambo wa Sudan kinachojulikana kama Rapid Support Forces (RSF) kimeongeza mashambulizi yake dhidi ya jiji la magharibi linaloshikiliwa na jeshi, al-Fashir, na kudhibiti “maeneo kadhaa ya makazi,” kwa mujibu wa tovuti ya habari inayoendeshwa binafsi ya Darfur24 iliyotoa taarifa jana.
“Video zilizothibitishwa na Darfur24 zinaonesha wapiganaji wa RSF wakidai kudhibiti maeneo kadhaa na sehemu muhimu ndani ya jiji hilo,” tovuti hiyo ilisema.
Jeshi limekanusha madai ya kusonga mbele kwa kikundi hicho, likisema kuwa wanajeshi wake wamekabiliana na mashambulizi yote ya RSF dhidi ya jiji hilo na kwamba “matokeo ya mapigano ya hivi karibuni hayajabadilika.”
Al-Fashir, ambayo ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na kitovu muhimu cha misaada ya kibinadamu, ndilo jiji kubwa zaidi katika eneo hilo ambalo bado lipo chini ya udhibiti wa jeshi.
RSF wamekuwa wakilizingira jiji hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kikundi hicho kimeshtumiwa kwa kuua na kuwateka raia waliokuwa wakijaribu kukimbia jiji hilo pamoja na kushambulia kambi za wakimbizi wa ndani zilizoko karibu.
Wakati huohuo, makundi ya wanaharakati wa Sudan yanajiandaa kuzindua kampeni ya kutaka muda wa ujumbe wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi hiyo yenye vita uongezwe kwa miaka miwili, kufuatia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea na hali mbaya ya kibinadamu, kwa mujibu wa tovuti ya Sudan Tribune yenye makao yake Paris.
Umoja wa Mataifa uliunda ujumbe huo mwaka 2023 ili kuchunguza ukiukwaji wa haki unaofanywa na jeshi na RSF.
Ujumbe huo unatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, wakati ambapo muda wake unatarajiwa kumalizika.
Isitoshe, Mtandao wa Madaktari wa Sudan unasema kuwa watu 46 wamefariki kutokana na utapiamlo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, huku wanawake wanaonyonyesha wapatao 19,000 wakihitaji msaada wa dharura wa lishe katika jimbo la Sudan la Kordofan Kusini.
Vifo hivyo vilitokea kati ya mwezi Julai na Agosti na waathirika wengi ni wanawake na watoto.
Mgogoro wa chakula unaoendelea Kordofan Kusini umetokana na mvutano unaoongezeka kati ya Sudan People’s Liberation Movement – North (SPLM-N) inayoongozwa na Abdelaziz al-Hilu na vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) ambao wanapigania udhibiti wa eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.
Mgogoro wa Sudan hadi sasa umesababisha vifo vya takriban watu 150,000 na kuwalazimu watu wengine milioni 12 kuyakimbia makazi yao.
0 Comments