Kampuni ya uzalishaji wa mbolea ya Minjingu Tanzania imefanya ziara katika Chama Kikuu cha Ushirika (IFCU) mkoani Iringa, ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha huduma kwa wakulima wa mkoa huo.
Akizungumza na Matukio Daima Media baada ya ziara hiyo, Bwana Shamba Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya Minjingu, Dkt. Mshindo Msolla, alisema kuwa dhamira kuu ya ujio wao ni kuimarisha uhusiano uliopo kati ya kampuni hiyo na IFCU, sambamba na kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima.
"Tumeanza kushirikiana na IFCU tangu msimu uliopita Leo tupo hapa kuangalia mafanikio tuliyopata, changamoto tulizokutana nazo na kupokea ushauri kutoka kwao. Pia tunakutana na wakulima ili kuwapa maelekezo ya mbinu bora za kilimo kwa mazao mbalimbali," alisema Dkt. Msolla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IFCU, Paul Mwinuka, alisema kuwa mahusiano yao na Minjingu yamekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima, hasa katika upatikanaji wa mbolea.
"Tumeanza kushirikiana nao tangu msimu uliopita kwa kupata baadhi ya mbolea kutoka kwao. Ziara hii inalenga kufanya tathmini ya msimu uliopita na kuweka mikakati mipya. Wakulima wa Iringa wategemee kupata mbolea nyingi na bora mwaka huu kutoka Minjingu," alisema Mwinuka.
Meneja wa IFCU, Tumaini Lupola, alieleza kuwa dhamira ya chama hicho ni kuchochea uzalishaji wa mazao kupitia vyama vya ushirika na kuwatafutia masoko ya uhakika.
"Msimu huu kwa mara ya kwanza tumesaidia wakulima wa zao la ufuta kuuza kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, jambo lililowapa faida kubwa. Kupitia ujio wa Kampuni ya Minjingu, tunawahakikishia wakulima upatikanaji wa mbolea bora kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji wao," alisema Lupola.
Ziara hiyo imeweka matumaini mapya kwa wakulima wa mkoa wa Iringa, hususan katika kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao yao kupitia ushirikiano wa karibu na Kampuni ya Minjingu.
0 Comments