Mwaka uliopita, Google imefanya mabadiliko, na pengine umeyaona. Jambo la kwanza unaloona katika matokeo ya utafutaji wako, mara nyingi ni jibu linalotolewa na akili ya mnemba (AI), badala ya orodha ya viungo (linki) kama ilivyozoeleka hapo awali kwenye Google.
Mwaka huu, watumiaji 900 wa intaneti huko Marekani, walitoa ruhusa kwa Kituo cha Utafiti cha Pew kufuatilia mitandao wanayotembelea.
Kulingana na uchambuzi mpya, watumiaji wa Google wana uwezekano mdogo wa kubofya linki za mitandao mengine, wanapoona muhtasari wa jawabu ya akili mnemba juu ya wanachokitafuta. 26% huacha kabisa kutafuta pindi tu akili mnemba inapowapa jawabu.
Hili ni jambo muhimu sana. Kwa ujumla watu huingia kwenye Google na kubonyeza linki mara bilioni tano kwa mwaka. Hapo ndipo shughuli nyingi za mtandaoni zinapoanzia.
Sehemu kubwa ya tovuti huzalisha mapato yao kupitia utangazaji wa matangazo ya biashara, hasa tovuti zinazotoa taarifa na maudhui badala ya kuuza bidhaa.
Tovuti nyingi zinahitaji watu kutoka Google ili kuendelea kufanya kazi," anasema Lily Ray, makamu wa rais wa taasisi ya kuboresha injini ya utaftaji na utafiti katika taasisi ya Amsive.
"Lakini muhtasari wa akili mnemba unapunguza watu kwa kiasi kikubwa kwenda kwenye tovuti nyingine na hilo limepunguza mapato kwa 20%, 30%, na hata 40%. Ina athari mbaya na kuondoa motisha kwa watu wengi kuunda maudhui."
Akili mnemba itaua tovuti?
Tovuti nyingi zinazochapisha maudhui hutegemea watumiaji wanaoingia kupitia viungo kwenye Google.
Kwa Google, hofu hiyo ni upuuzi: "Tunashuhudia watu wakiingia kwenye tovuti kwa mabilioni kila siku na hatujaona kushuka kwa kiasi kikubwa kwa wingi wa watu katika tovuti, kama inavyopendekezwa," msemaji wa Google amesema.
"Utafiti huu unatumia mbinu mbovu na seti ya maswali yenye upendeleo ambayo hayawakilishi uhalisia."
Lakini Pew inasema ina uhakika katika utafiti wake. "Matokeo yetu kwa kiasi kikubwa yanaendana na tafiti huru zilizofanywa na kampuni nyingine," anasema Smith.
Ripoti nyingi zinaonyesha kuwa majibu ya akili mnemba hupunguza idadi ya watu wanaoingia kwenye tovuti kwa 30% hadi 70%, kwa kuzingatia kile mtafutaji anachotafuta.
Lakini Google inaiambia BBC kuwa utafiti huo haipaswi kutiliwa maanani. Kampuni hiyo inadai kuwa wingi wa watu katika wavuti hubadilika kwa sababu nyingi.
Msemaji wa Google anasema kutumia jawabu za akili mnemba ni bora, kwani watumiaji hupoteza muda mwingi kwenye tovuti wanazotembelea.
Kinachoshangaza ni kwamba akili mnemba ya Google yenyewe haikubaliani na idara yake ya matangazo ya Google
Ukiuliza Google Gemini, itakuambia kuwa jawabu za akili mnemba ni hatari kwa tovuti.
Na kulingana na Ray, ushahidi uko wazi: "Google inajaribu kudanganya na kuficha ukweli kwa sababu haitaki kuwatia hofu watu.”
Akili mnemba inavutia
Hapo awali, Google ilitoa viungo kujibu maswali.
Watu wanavutiwa zaidi na akili mnemba katika utafutaji na inawaruhusu watumiaji kuuliza maswali zaidi. Lakini Raya ana mtazamo tofauti.
“Maelezo ya jumla ya akili mnemba mara nyingi huwaibia watumiaji uwezo wao wa kuchanganua taarifa tofauti, kuchagua wanachotaka kusoma, na kufikia hitimisho lao,” anasema.
Google inadai kuwa majibu ya AI ni ya manufaa na yenye lengo kutoa usahihi, urahisi zaidi, kutumia muda mchache, na kuwa na machaguo kidogo.
Lakini ikiwa Google itafanya makosa na tovuti kuanza kutoweka, haitakuwa kwa sababu tulibofya kiungo kisicho sahihi. Itakuwa kwa sababu tuliacha kubofya kabisa.
0 Comments