Header Ads Widget

JIKO LA MKAA LASABABISHA VIFO VYA WATOTO WATATU BUSEGA.

 



Na Matukio Daima App, Busega.


WATOTO watatu wa jinsia ya kike, wakazi wa kijiji na kata ya Mkula, Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu, wamefariki dunia kwa kukosa hewa wakiwa wamelala ndani ya hema ambalo kulikowemo na jiko la mkaa ambalo lilikuwa limewashwa moto.


Watoto hao wamefikiwa na umauti, Agosti 18, 2025 wakati wakiwa kwenye makambi ya waumini wa Kanisa la Waadventisti wasabato ambayo yalikuwa yanafanyika kwenye kanisa la Wasabato kijijini hapo.


Mashuhuda wa tukio hilo wamewaeleza waandishi wa habari kuwa, watoto hao wakiwa kwenye makambi hayo siku hiyo ya tukio, waliamka asubuhi kisha wakawasha jiko la mkaa kwa ajili ya kupika uji wa kunywa.


Lukasi Mashauri mmoja wa washuhuda hao amesema kuwa baada ya kuwasha jiko hilo walilichukia na kuliingiza katika hema (Tenty) ambalo walikuwa wanalala kwenye makambi hayo.


“ Baada ya kuwasha jiko na kuliingiza ndani na kwa sababu siku hiyo kulikuwa na mvua inanyesha wakaamua kuingia ndani na wao, wakaanza kupika uji huku wakiwa wamelifunga hema hilo,” amesema Mashauri.


Naye Revocatus Vedastus amesema kuwa wakati watoto hao wakiendelea kupika uji, walipitiwa na usingizi huku hema likiwa limefungwa lote na kukosa hewa safi.


“ Kuna mtoto mwingine ambaye aliamka asubuhi yeye akaondoka kwenda shule, yule mtoto baada ya kurudi kutoka shule akalifungua hilo hema ndipo akakuta wenzake wote watatu wamelala na kuwaamsha wakawa hawaitiki,” Amesema Vedastus.


Mwenyekiti wa kitongoji cha Sokoni katika kijiji hicho Bahati Manyanza, amesema kuwa baada ya mtoto huyo kugundua tukio hilo, waliamua kuwakimbiza watoto hao katika hospitali ya Mkula wilayani humo.


“ Baada ya kuwapeleka hospitali tuliambiwa tayari wamefariki, na sababu kubwa ni kukosa hewa wakiwa ndani ya hema hilo na huku wakiendelea kuwasha jiko la mkaa lenye moto,” amesema Manyanza.


Akidhibitsha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amekiri kutokea kwa tukio hilo, huku akieleza kuwa chanzo ni jiko la mkaa ambalo watoto hao waliliwasha kisha kuingia nalo ndani ya hema.


Macha amesema kuwa baada ya kuingia nalo ndani watoto hao walianza kupika uji, ambapo walipitiwa na uzingizi huku hema likiwa limefungwa na kusababisha hewa chafu kusambaa.


Amewataja watoto hao kuwa ni Loveness Kilonzo (09) Mwanfunzi wa Darasa la tatu, Pasheni Yusuph (14) Mwanafunzi wa darasa la saba, na Mary Jackson (12) wote wanafunzi wa shule ya Msingi Masangani.


“ Tunatoa pole sana kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao, ni tukio la kusikitisha sana, kilichotokea tunaweza kusema ni ajali ambayo imetokea kwa bahati mbaya na kutokujua, na makambi hayo kama serikali huwa tunayatambua,” amesema Macha.


Ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo, uongozi wa kanisa kwa kushirikiana na serikali waliamua kusitisha uwepo wa kambi kwenye kanisa hilo na kukubaliana kuwa watakaa kwa mara nyingine na kuitisha upya.


Macha ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa kanisa hilo, kuhakikisha wanatoa taarifa kwa serikali ili kuweza kuhakikisha mazingira ya uwepo wa makambi hayo yanakuwa sawa na rafiki kwa waumini.


“ Ukweli ni lazima tuseme kuwa uzembe ulifanyika, hilo hatuwezi kuficha, tunawaomba na kuwasisitiza kuwa tukio hilo liwe fundisho kwa wote, kuwepo na taarifa kwa serikali ili kuweza kuhakikisha mazingira ya makambi yanakuwa salama,” amesema Macha.


Mwisho.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI