Na mwandishi wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemteua Dkt. Samia
Suluhu Hassan kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho na Dkt. Emmanuel Nchimbi katika
nafasi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza leo Jumatano, Agosti 27, 2025 jijini Dodoma,
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, amesema wagombea
waliopendekezwa na CCM wametimiza masharti yote ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, hivyo kuthibitishwa rasmi kuwania nafasi hizo.
“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inawateua Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Katika hatua nyingine Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi ameendelea na ukaguzi wa maandalizi ya uzinduzi wa kampeni za CCM katika Viwanja vya Tanganyika Packers, ambapo shughuli mbalimbali zinaelekea kukamilika.
Ambapo CCM inatarajia kuzindua rasmi kampeni zake katika viwanja hivyo siku ya Alhamisi, tarehe 28 Agosti 2025.Uzinduzi huo utaongozwa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, akiambatana na Mgombea Mwenza, Dk. Emmanuel John Nchimbi, pamoja na viongozi wa Chama na Jumuiya zake.
0 Comments