Msafara wa mgombea wa Urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, umekumbana na kizuizi cha kuingia katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) mjini Dodoma leo, wakati wagombea kutoka vyama mbalimbali walipofika kurejesha fomu zao.
Mpina, ambaye hivi karibuni alihama kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada
ya kushindwa katika kura za maoni za ubunge Jimbo la Kisesa, alijiunga na ACT
Wazalendo na kuomba kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Hata hivyo, uamuzi wa chama hicho kumteua umeibua mtazamo tofauti ndani na
nje ya chama, baada ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo, Monalisa
Ndala, kupinga uteuzi huo akidai kanuni za chama zimekiukwa. Katika barua
aliyomwandikia Katibu Mkuu wa chama, Ado Shaibu, Monalisa alieleza kuwa Mpina
hajakidhi kanuni za kudumu za chama toleo la mwaka 2015, hususan kanuni namba
16 (4) (iv) inayomuhitaji kuelewa itikadi, falsafa, misingi na sera za chama.
Kutokana na pingamizi hilo, Siku ya jana Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC,
Ramadhan Kailima, alimwandikia barua Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo akieleza kuwa
tume hiyo, kupitia barua yake ya awali ya Agosti 15, 2025, ilieleza kuwa Mpina
hatapaswa kufika katika Ofisi za Tume kwa ajili ya uteuzi uliopangwa kufanyika
Agosti 27, 2025.
Baada ya barua hiyo, ACT Wazalendo ilitoa taarifa ikipinga uamuzi wa Msajili
wa Vyama vya Siasa wa kutengua uteuzi wa Mpina, ikieleza kuwa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa chama inaendelea kupitia hatua hiyo kwa umakini na itatoa
mwelekeo wake wa kina katika muda muafaka.
0 Comments