Na Matukio Daima Media
WAKALA wa Elimu Nje ya Nchi Global Education Link (GEL) inatarajia kusafirisha wanafunzi zaidi ya 1,000 kwenda kusoma kozi mbalimbali nje ya nchi na imeanza kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kuwatumia wanafunzi wanaosoma nje ya nchi kutangaza utalii.
Hayo yalisemwa jana jijjini Dar es Saaalaam na Mkurugenzi Mkuu wa (GEL), Abdulmalik Mollel, wakati wa kuzungumza na wazazi na wanafunzi wanaotarajiwa kusafiri siku za hivi karibuni kwenda masomoni nje ya nchi.
Katika hafla hiyo pia wanafunzi hao walipewa elimu ya mambo ya kufanya na ambayo hawapaswi kufanya wakiwa masomoni nje ya nchi na walipewa nyaraka mbalimbali muhimu za kusafiri nazo kama hati ya kusafiria tayari kwa safari hiyo.
Mollel alisema kwa kawaida safari kama hizo huwa zinaanza mwezi wa nane hadi wa kumi na siku ya Jumamosi wanafunzi 100 wanaoondika waliwapewa Visa wale wanaotarajia kuondoka tarehe 27 mwezi huu.
“Kwa mwezi wa nane tarehe 27 wataondoka wanafunzi 100, tarehe10 mwezi wa tisa wataondoka wanafunzi 113, tarehe 21 mwezi wa tisa wataondoka wanafunzi 100 na tarehe 25 mwezi wa tisa wataondoka wanafunzi 117 kwa hiyo kila wiki wanafunzi wataondoka,” alisema na kuongeza.
“Kwa uchache tunatarajia kuwa na wanafunzi 800 watakaoondoka nje ya nchi kwa masomo kuanzia mwezi wa nane na wa tisa na mwezi wa kumi…. Nchi kama India, Cyprus, Uingereza mwezi wa kumi wanakuwa wamefunga udahili kwa hiyo tutaendelea kupeleka wanafunzi nchi za Malaysia, Dubai, Canada, Marekani na China hizi nchi zinaruhusu wanafunzi kwenda hata mwezi wa 11,” alisema Mollel
Mollel alisema GEL imekubaliana na Bodi ya Utalii nchini (TTB), kuendelea kushirikiana kutangaza utalii na kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye maeneo mbalimabli nchini.
Alisema ushirikiano huo utahusisha vijana wa Kitanzania wanaopata fursa za kusoma nje ya nchi kupitia taasisi ya Global Education Link ambapo vijana watafundishwa kuhusu vivutio vya utalii na nyanja za uwekezaji zilizopo nchini,.
Alisema elimu watakayopewa itawasaidia wanapokuwa masomoni nje ya nchi wawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kimataifa.
Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nassor Garamatatu, aliwataka vijana hao kutangaza vivutio mbalimbali vya uwekezaji vilivyoko Tanzania kwa muda wote watakapokuwa masomoni.
Alisema Tanzania inahitaji watalii wengi wa kutembelea kwenye vivutio vilivyoko kwenye mbuga mbalimbali kama Mikumi, Serengeti, Ngorongoro Manyara hali ambayo italiingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
“Mtapata marafiki wanaotoka kwenye familia zinazopenda kusafiri safari kwenye maendeo mbalimbali duniani muwashawishi waje hapa Tanzania kwasababu mtakuwa mmetimiza wajibu wenu kama mabalozi, mheshimiwa Rais ameanzisha na sisi wa chini mkiwemo wanafunzi mnapaswa kumuunga mkono,” alisema Garamatatu.
“TTB tutatafuta muda siku nyingine mkirudi tutawapangia safari nyinyi wanafunzi mkatembelee vivutio vya utalii, mkifahamu vizuri kuhusu utalii uliopo nchini mtaweza kufanya vizuri kwenye kuitangaza nchi yenu huko mnakoenda,” alisema
“Huko mnakokwenda mnaenda kuchangamana na dunia, mtakutana na wanafunzi wa mataifa yote duniani kwa hiyo tumieni hiyo fursa kufanyakazi ya kuitangaza nchi yako ili ipate fedha nyingi za kigeni ambazo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema Garamatatu.
Baadhi ya wazazi waliohudhuria mkutano huo waliipongeza GEL kwa huduma, malezi na mwongozo bora kwa vijana wanaojiandaa kwedba usoma nje ya nchi.
“Hii ni kazi kubwa sana, siyo rahisi kwa mzazi kuifanya kwa hiyo mmeturahishia sana mnastahili pongezi kwa kazi hii ya kuwahudumia watoto wetu kwasababu licha ya kuwasimamia kuwasafirisha mpaka vyuoni pia mnawafuatilia kitaaluma mpaka wanapomaliza,” alisema Vicent Razak.
Kwenye mkutano huo NBC na Global Education Link waelimisha wanafunzi hao kuhusu matumizi ya fedha kidigitali nje ya nchi ili kupunguza makato na usumbufu wa kibenki.
Mwisho
0 Comments