Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney ametangaza kuwa nchi yake inapanga kulitambua rasmi Taifa la Palestina, katika kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kitakachofanyika mwezi Septemba, 2025.
Tangazo la Carney laashiria mabadiliko makubwa ya sera kwa Canada, ikiungana na Ufaransa na Uingereza kama taifa la tatu miongoni mwa mataifa saba tajiri zaidi duniani, G7 kuunga mkono utambuzi wa taifa la Palestina, huku vita vikizidi kuighubika Gaza.
Hali ya kibinadamu inazidi kuzorota Gaza
Carney amesema hatua hiyo inachochewa na kuzorota kwa hali ya kibinadamu Gaza na kufifia kwa matumaini ya suluhisho la mataifa mawili. Waziri Mkuu huyo wa Canada amekosoa vikali mashambulizi ya Hamas, upanuzi wa makaazi ya walowezi, na hatua ya Bunge la Israel kutaka kulinyakua eneo la Ukingo wa Magharibi, akisema mfumo wa sasa wa amani hauwezi tena kutekelezeka.
Israel imelaani vikali uamuzi wa Canada, ikisema ni zawadi kwa "ugaidi wa Hamas" kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7, 2023. Ubalozi wa Israel mjini Ottawa umeishutumu Canada kwa kuhalalisha vitendo vya kigaidi. Kwa upande mwingine, Rais Mahmoud Abbas amepongeza hatua hiyo akisema ni "ya kihistoria,” huku Ufaransa ikielezea nia ya kushirikiana na Canada kufufua juhudi za amani za kikanda.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameonesha hasira kutokana na hatua hiyo, akisema inaweza kuvuruga mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na Canada. Ametishia kuiwekea Canada ushuru wa asilimia 35 kwa bidhaa zisizo ndani ya mkataba wa USMCA, akionya kuwa "itakuwa vigumu sana” kufikia makubaliano ya kibiashara na Canada.
Wakati hayo yakijiri, serikali ya Ujerumani kupitia muungano unaoongoza imeongeza shinikizo kwa Israel kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.
Ujerumani yataka hatua madhubuti zichukuliwe
aibu Kiongozi wa wabunge wa chama cha Social Democratic, SPD, Siemtje Möller, amesema ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe, na kwamba silaha hazipaswi kutumika katika operesheni zinazokiuka sheria za kimataifa. Ameongeza kuwa Ujerumani inataka mazungumzo ya amani, Hamas kusalimisha silaha, na kusitishwa kwa ujenzi wa makaazi haramu katika Ukingo wa Magharibi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, amesafiri kuelekea Israel kushinikiza makubaliano ya kusitisha mapigano na kuimarisha hali ya kibinadamu Gaza. Anatarajiwa kufanya mazungumzo na maafisa wa Israel pamoja na wale wa Mamlaka ya Palestina.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Sweden, Ulf Kristersson, ameutaka Umoja wa Ulaya kusitisha mara moja baadhi ya vipengele vya makubaliano ya kibiashara kati yake na Israel, akilalamikia namna Israel inavyoendesha operesheni zake za kijeshi Gaza.
0 Comments