Header Ads Widget

ACT YAJIPANGA KUSHIKA DOLA YATUMA SALAMU KWA CCM


Na Matukio DaimaApp 

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimejipanga kwa umakini mkubwa kuhakikisha kinakiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2025.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 6, 2025 na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama unaoendelea katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Shaibu amesema ACT Wazalendo imejifunza kutokana na uzoefu wa historia ya vyama vingi nchini, kuanzia miaka ya 1990 hadi sasa. 


Amesema kuwa tangu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ACT Wazalendo imekuwa ikiweka mkazo mkubwa kwenye mipango ya kimkakati, ikitathmini mambo yaliyofanywa vyema na wapinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, sambamba na kufanyia kazi maeneo ya udhaifu ambayo yamekuwa kikwazo kwa upinzani kwa miaka mingi.

Ado amesema chama chake kipo tayari na kina "silaha za kutosha" kisiasa, kimaadili na kimkakati, kuhakikisha mabadiliko ya uongozi wa nchi yanapatikana kwa njia ya kidemokrasia.

Naye, Mwenyekiti wa Chama hicho, Othman Masoud Othman, amesema kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho si mkutano wa kawaida, bali ni hatua muhimu ya kurejesha sauti, mamlaka na utu wa Mtanzania, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinyimwa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa nchi yao.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema kuwa jukumu lake la kikatiba ni kufungua mkutano, nuzito wa mkutano huo.

“Mkutano huu unakwenda kutengeneza ramani ya kuwapatia Watanzania kwanza sauti zao, ambazo zimekabwa, zimenyimwa na zimezuiwa kwa muda mrefu,” amesema Othman.

Amesisitiza kuwa mkutano huo haujaitishwa kwa lengo la kupanga miundombinu ya uchaguzi au kutafuta kura kwa ajili ya chama, bali ni kuandaa utaratibu mpya wa kurejesha mamlaka mikononi mwa wananchi, mamlaka ya kuchagua na kuwawajibisha viongozi wao.

“Binadamu yeyote aliyenyimwa sauti hizi mbili, ya kumuweka kiongozi na ya kumwajibisha kiongozi huyo anaishi utumwani hata kama anaishi katika kasri lenye raha,” ameongeza.

Amewaonya wajumbe na viongozi waliohudhuria mkutano huo wasije wakawa

 sehemu ya kuwasaliti wananchi kwa kukosa maono ya mabadiliko au kushindwa kutekeleza wajibu wao.

"Tusiwaangushe Watanzania. Mkutano huu si wa kutengeneza wagombea, si wa kutafuta kura za ACT Wazalendo, tunajenga mwelekeo wa kisera na kisiasa wa kuwaondoa Watanzania kwenye utumwa wa kukosa ushawishi juu ya mustakabali wao,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu akizungumza katika Mkutano huo wamechagua kushiriki uchaguzi sio kwa sababu ya mapenzi bali kwa sababu ya dhamira ya kuwaletea wananchi maslahi.

"Ninataka niweke wazi mbele ya wajumbe wote, hatukuchagua kushiriki uchaguzi kwa sababu ya mapenzi, tumechagua kushiriki kwa sababu ya dhamira, dhamira ya kulinda haki ya kuchagua, dhamira ya kurejesha thamani ya kura ili wananchi wawe na uwezo wa kuamua nani awe Kiongozi wao." amesema Semu na kuongeza,

"Tumejifunza kutokana na historia, kususia hakujawahi kuleta mabadiliko, mapambano ya kweli ni ya wale wanaojitosa uwanjani. Na sisi, ACT Wazalendo, tumeingia vitani na tutatoka na ushindi! Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia ipasavyo uchumi, huduma za jamii, na masuala ya utawala bora,".

Semu ameongeza "Watanzania wengi wanaishi katika umaskini, ukosefu wa ajira na uhakika wa vipato, wakiwa hawana huduma bora za kijamii, wakiishi kwa hofu, wakizuiwa kupaza sauti na kupewa matumaini hewa ya kesho iliyo njema, tumeendelea kuwa taifa la wachache kunufaika na walio wengi kuteseka," 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI