Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, ameipongeza Wizara pamoja na taasisi na idara zake kwa ubunifu mkubwa unaosaidia kuvutia wananchi na watalii wa ndani kutembelea vivutio vya utalii nchini.
Akizungumza Julai 12, 2025, alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Saba Saba), Dk. Chana alisema banda hilo limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wananchi kutokana na huduma na taarifa mbalimbali zinazotolewa na taasisi na idara zake.
“Nimepokea taarifa kwamba wananchi wengi wametembelea banda la Wizara, jambo linalothibitisha ubunifu mkubwa katika kutoa elimu kuhusu uhifadhi na vivutio vyetu,” alisema Dk. Chana.
Aidha, Waziri amewahimiza wananchi kuendelea kutembelea vivutio vilivyopo nchini, akisisitiza kuwa utalii wa ndani umekuwa ukikua hususan katika misimu ya sikukuu na matamasha kama haya ya Saba Saba kutokana na ofa na huduma zinazotolewa.
Dk. Chana alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha miundombinu inayowezesha watalii kufika kwa urahisi kwenye hifadhi na vivutio vya asili.
“Tunapaswa kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais kupitia filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania, ambazo zimechangia kwa kiwango kikubwa kutangaza utalii wetu ndani na nje ya nchi,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri, filamu hizo zimechangia kuongeza idadi ya watalii, hatua inayosaidia kukuza kipato cha wananchi na pato la Taifa kwa ujumla.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa mabalozi wazuri kwa kuitangaza Tanzania na kutumia elimu wanayopewa na wataalamu wa uhifadhi ili kulinda misitu na maeneo yote yaliyohifadhiwa.
“Nawaomba wadau na wananchi wasibaki tu kwenye maonesho ya Saba Saba, bali pia waendelee kutembelea hifadhi za misitu na vivutio vingine, mfano hifadhi za misitu ya asili chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bi. Latifa M. Khamis, aliipongeza Wizara na idara zake kwa kuongoza kwa kuwa na wageni wengi zaidi ya 600,000 waliotembelea banda hilo na kupata elimu ya uhifadhi na utalii.
Alibainisha kuwa TanTrade inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuimarisha miundombinu na kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zinazotolewa kupitia maonesho hayo.
0 Comments