Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAZIRI wa maji Jumaa Aweso amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kusimamia kwa karibu miradi ya maji na kuwakemea na kuchukua hatua kwa wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati.
Waziri Aweso ametoa maagizo hayo alipofanya ziara kutembelea na kukagua mradi wa maji wa mji wa Kasulu mkoani Kigoma wenye thamani ya shilingi Bilioni 35 ambao ni moja ya miradi inayotekelezwa katika miji 28 nchini.
Katika hilo Waziri huyo alisema kuwa serikali imeweka dhamira ya dhati kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa kila Mtanzania hasa wanawake waliokuwa wakiteseka kutafuta maji hivyo kutafuta fedha ambazo tayari zimeelekezwa kwa wakandarasi hivyo hakuna sababu ya miradi hiyo kushindwa kutekelezwa kwa wakati.
Waziri Aweso Akitoa maagizo kwa mkandarasi wa mradi huo, Serico Co.Ltd, Robert Kisanga amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha kazi kwa wakati kwa fedha amepewa lakini hawalipi wafanyakazi wake hivyo wafanyakazi wengi kukimbia na mradi kusuasua na kutokana na hilo amemtaka Mkuu wa wilaya Kasulu, Isack Mwakisu kumsimamia mkandarasi huyo na afanye kazi usiku na mchana.
Awali akitoa maelezo ya mradi kwa waziri wa maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji ya mji wa Kasulu, Mhandisi Hussein Nyemba alisema kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi Bilioni 35 utakapokamilika utahudumia jumla ya watu 187,343 kutoka kata 13 za mji wa Kasulu mkoani Kigoma.
Nyembaa alisema kuwa kwa sasa mradi umefikia asilimia 49 ya utekelezaji wake malengo yakiwa ni kuhakikisha mradi unatarajia kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu ambapo kukamilika kwake kutawezesha lita za maji milioni 15 zitazalishwa na kuwezesha maji kupatikana kwa asilimia 100 kutoka asilimia 71 za sasa .
0 Comments