Header Ads Widget

UBAGUZI WA RANGI UMEONGEZEKA KATIKA SOKA LA WANAWAKE – ASEMA BEKI WA ENGLAND

 

Lucy Bronze

Beki wa England, Lucy Bronze amesema kukua kwa soka la wanawake kunaenda sanjari na ongezeko la unyanyasaji wa kibaguzi dhidi ya wachezaji wakati huu mchezo huo ukivuta mashabiki zaidi.

Bronze, ambaye alikuwa ufunguo wa ushindi wa England wa robo-fainali dhidi ya Sweden kwenye Euro 2025 siku ya Alhamisi, alifanya mkutano na waandishi wa habari wenye hisia baada ya mchezaji mwenzake Jess Carter, ambaye ni Mweusi, kutangaza kuwa amekuwa akilengwa na matusi ya ubaguzi wa rangi tangu michuano hiyo ilipoanza.

"Kadiri mchezo wa soka unavyokuwa, ndivyo kelele zinavyoongezeka, mashabiki wanavyoongezeka, na wakosoaji wanaongezeka," amesema Bronze.

"Hatuna tatizo na wakosoaji - ndiyo maana tunapenda mchezo - lakini hatuko tayari kudhalilishwa. Hasa katika soka la wanawake, unyanyasaji wa mtandaoni unaonekana kuwa mbaya zaidi na zaidi.

"Ni jambo ambalo tunalifahamu sana. Kuna namna ya kufanya mabadiliko. Kuna suluhisho. Sina jibu, lakini nina uhakika kuna suluhisho."

Bronze aliulizwa kama matusi dhidi ya Carter yatawafanya wachezaji wengine wachanga Weusi kufikiria mara mbili mbili kuhusu kuichezea England.

"Natumai wachezaji hao wanajua kuwa hata wapitie nini, wataungwa mkono na timu hii, kwamba hatupendi vitendo hivi, tunataka mabadiliko, sio tu katika mpira wa miguu, lakini katika jamii, wanaelewe wachezaji wachanga kuwa wanaweza kukua na kuwa mashujaa katika timu ya England," alisema.

Uingereza itacheza na Italia katika nusu fainali siku ya Jumanne mjini Geneva.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI