Na Mwandishi wa NCAA, DSM
Waziri wa Maliasili na Utalii mhe. Balozi Dkt.Pindi Chana (mb) amewapongeza watendaji wa wizara hiyo kwa kutimiza malengo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kufikisha idadi ya watalii milioni tano kama ilivyoainishwa kwenye ilanı ya chama hicho.
Dkt.Chana ametoa pongezi hizo katika uzinduzi wa siku maalum ya Ngorongoro (Ngorongoro Day) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya maonesho ya 49 ya biashara ya kimataifa Sabasaba yanayoendelea Dar Es Salaam.
“Niwapongeze sana watendaji wenzangu wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa sekta ya utalii kwani ilanı ya CCM ilitutaka tufikishe watalii milioni tano na sasa tunatembea kifua mbele kwani idadi hiyo imetimia.
Waziri Chana pia ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa kukusanya shilingi bilioni 269.9 kutoka lengo la shilingi bilioni 230.
Akitoa maelezo ya siku hiyo ya Ngorongoro Meneja wa huduma za utalii na Masoko Bi Mariam Kobelo amesema lengo kubwa ni kuunga mkono juhudi za mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii na kupata wageni wengi zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania Ephraim Mafuru amesema bodi hiyo kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na utalii zitaendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa idadi ya watalii na mapato ya serikali kupitia sekta hiyo yanaongezeka.
0 Comments