Na Shemsa Mussa -Kagera
Kiasi cha Mkopo wa shilingi bilioni 1.5 umetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwaajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na zana bora za uvuvi kwa wavuvi na wafugaji Mkoani Kagera.
Akizungumza katika mafunzo kwa wafugaji na wavuvi, Mkuu wa Mkoa Kagera Bi Hajjat Fatma Mwassa amesisitiza kuzingatia elimu na mafunzo ya ufugaji wa samaki wanayopewa na wataalamu huku akisema serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ufugaji huo wa njia ya vizimba na lengo ikiwa ni wananchi kujikomboa kimaisha,kutokomeza umaskini na kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
"Niwambie tu Serikali ya Awamu ya Sita imetoa mikopo ya shilingi milioni 10 kwa kila kizimba kwa ajili ya uendeshaji,na sisi kama mkoa yametengwa maeneo 12 yanayofaa kwaajili ya vizimba vya samaki na tayari vimba 52 vimesimikwa mpaka sasa"
Wananchi zaidi ya 140 mkoani Kagera wamehudhuria mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuongeza uzalishaji wa samaki kutoka tani 32,349 zinazozalishwa kwa sasa,na kuwa kizimba kimoja chenye ukubwa wa mita za mraba 256 kina uwezo wa kuzalisha tani 14 kwa muda wa miezi saba.
Mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba yanafanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera kwa siku mbili Julai 10 hadi 11, 2025 na yanaendeshwa na wataalam kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi .
0 Comments