Header Ads Widget

TABORA YAPIGA HATUA SEKTA YA ASALI VIWANDA 4 VYAJENGWA ,UZALISHAJI WAONGEZEKA

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha, amesema kuwa mkoa huo umeendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya uzalishaji wa asali na uhifadhi wa mazingira, hali inayochochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima na kuimarisha thamani ya asali ya Tabora kitaifa na kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 11 2025 wakati akieleza mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita kwa mkoa huo,  amesema,hadi kufikia mwaka 2025, viwanda vinne (4) vya kisasa vya kuchakata na kufungasha asali vimejengwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuongeza thamani ya zao hilo.

 “Mwaka 2020 tulikuwa na uzalishaji wa asali tani 1,868.6, lakini sasa tumefikia tani 2,002.48 kwa mwaka 2025,hii ni hatua kubwa inayotokana na mikakati ya mkoa katika kuwajengea uwezo wafugaji wa nyuki na kuvutia uwekezaji kwenye sekta hii,” amesema Chacha.


Aidha, ameongeza kuwa mafanikio hayo yameenda sambamba na juhudi za uhifadhi wa mazingira, ambapo misitu ya hifadhi ya vijiji imeongezeka kutoka misitu 6 yenye ekari 11,952.5 mwaka 2020 hadi misitu 37 yenye ukubwa wa ekari 330,780.75 mwaka 2025.

 “Kuongezeka kwa misitu ya hifadhi ya vijiji ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya serikali, wananchi na wadau wa mazingira, hii inalinda vyanzo vya uzalishaji wa asali na kuongeza kipato kwa jamii,” ameeleza.


Mkuu huyo wa mkoa amehimiza wakazi wa Tabora kuendelea kutumia fursa ya sekta ya asali kwa njia endelevu na kuwataka wawekezaji zaidi kujitokeza, akisema Tabora iko tayari kwa ushirikiano wa kibiashara.

 “Asali ya Tabora ni bidhaa ya kimkakati, na tunalenga kuifikisha mbali zaidi katika masoko ya kimataifa, Tunawakaribisha wawekezaji kushirikiana nasi kukuza sekta hii,” amesisitiza Chacha.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI