Header Ads Widget

POLISI MWANZA WAKAMATA MTANDAO WA WIZI WA SAMAKI VIZIMBANI

 

Na Chausiku said 

Matukio Daima Media Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa samaki wanaofugwa kwenye vizimba katika mialo ya Nyambilo, Kongoro, Chabula na Kitongosima, wilayani Magu.

Tukio hilo lilitokea Julai 18, 2025 majira ya saa 12 jioni, ambapo askari wa Kikosi cha Wanamaji kwa kushirikiana na askari wengine walifanya doria maalum ndani ya Ziwa Victoria kwa lengo la kudhibiti matukio ya wizi wa samaki yanayofanywa na baadhi ya wavuvi wasio waaminifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 21, 2025 jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa alisema watuhumiwa waliokamatwa ni Elikana Jeremiah (47) mfanyabiashara wa samaki na mkazi wa Mwabui Nyanguge; Samba Mwambala (41) mkazi wa Mahina Nyakato; Mganga Kabere (49) mvuvi kutoka Nyambiro Nyanguge; Kapili Nzali (21) mkazi wa Mwamayombo Nyanguge na Joseph Pagwa (61) mkazi wa Kijiji cha Lutale.

“Kikosi chetu kilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao waliokuwa wakijihusisha na wizi wa samaki kwenye vizimba na kuwauza kwenye masoko kama mali yao halali,” alisema DCP Mutafungwa.

Katika oparesheni hiyo, polisi walikamata vielelezo ikiwemo samaki 89 wa aina ya sato, jokofu moja la kuhifadhia samaki, pamoja na mtumbwi wenye namba za usajili TZ MUM 6943 unaosadikiwa kutumika kwenye vitendo vya uhalifu huo

DCP Mutafungwa alieleza kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakidai kuwa samaki hao ni wa kwao kwa kuwa wanaogelea kwenye ziwa, hivyo kuvua kwenye vizimba si kosa — madai ambayo polisi wamesema hayana msingi wa kisheria.

“Tunapenda ieleweke kuwa uvuvi unaruhusiwa kwa mujibu wa sheria, na hata wawekezaji wa vizimba nao wanaruhusiwa kuendesha shughuli hizo kwa kufuata taratibu. Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha hakuna mvuvi anayemwibia mvuvi mwingine,” alisisitiza Kamanda Mutafungwa.

Polisi wameahidi kuendeleza doria katika maeneo ya ziwa ili kuimarisha ulinzi na kulinda uwekezaji wa vizimba unaochangia pato la jamii na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI