![]() |
Waziri Prof Kabudi |
Na. Mwandishi Wetu, Chamwino.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha la Utamaduni wa kabila la Wagogo "Cigogo Music Festival 2025" ambalo mwaka huu ni la msimu wa 16, linalofanyika kila mwaka katika Kijiji cha Chamwino Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa Umma, Mratibu wa Tamasha hilo linaloandaliwa na Kituo cha Sanaa na Utamaduni Chamwino- Chamwino Arts Centre (CAC); Bw. Sospeter Mapana amesema maandalizi yote yamekamilika ambapo tamasha litafanyika kuanzia Ijumaa tarehe 25 hadi Jumapili ya terehe 27 Julai mwaka huu katika viwanja vya Mshikamano, Chamwino Ikulu, Dodoma huku mgeni rasmi kwa mwaka huu, akitarajiwa kuwa Mhe Waziri Prof. Kabudi.
"Uongozi wetu unaendeleza ushirikiano madhubuti kati ya CAC na Serikali katika
juhudi za kuendeleza urithi wa kitamaduni na kukuza sekta ya sanaa kwa maendeleo endelevu.
Katika miaka ya nyuma, tamasha hili limepata heshima ya kuwa na wageni rasmi mawaziri wa sekta ya Utamaduni na Sanaa, akiwemo Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma (2024) na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (2023).
Tamasha la mwaka huu, ambalo ni la mwaka wa kumi na sita(16) tangu kuanzishwa, linatarajiwa kuwa na mvuto wa kipekee likiwa ni jukwaa muhimu la kuenzi na kuendeleza tamaduni za Wagogo na zaidi ya makabila 100 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, kupitia muziki wa asili, ngoma na sanaa za kitamaduni.
“Ni fahari kubwa kutangaza kuwa Waziri wetu mpendwa, Mhe. Prof. Kabudi, atakuwa mgeni rasmi. Tamasha hili si burudani tu, bali ni fursa ya mafunzo, majadiliano, usajili wa wasanii kupitia BASATA na COSOTA, pamoja na elimu ya fedha kutoka kwa taasisi mbalimbali za kifedha zitakazoshiriki,” amesema Mratibu wa Tamasha, Bw. Sospeter Mapana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chamwino Arts Centre (CAC), Bw. Naamala Samson, amewataka wananchi, wanaharakati wa utamaduni na wadau wote wa sanaa kujitokeza kwa wingi, kwani tamasha hilo limekuwa tukio muhimu katika kalenda ya kiutamaduni nchini.
Ambapo mwaka huu zaidi ya vikundi 50 vya utamaduni vinatarajiwa kushiriki, vikileta pamoja wasanii zaidi ya 1,000.
"Tunatarajia kuwa na ugeni mkubwa kuanzia Ijumaa tarehe 25 Julai, wa Vikundi na watu mbalimbali.
Lakini pia maonyesho na burudani yatakuwa yanaana kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni siku ya Jumamosi na Jumapili na hakutakuwa na kiingilio, hivyo tunawakaribisha kwa moyo wote.” Amesema Bw. Samson.
Aidha, Bw. Samson aliwashukuru wadhamini na wahisani waliokwisha jitokeza, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo; Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chamwino Connect, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya CRDB, FEGY BRAND, Gen 2 K, Picha Zina Sauti, Connect Creative Hub, Shusha Stress na wengine mbalimbali.
Chamwino Arts Centre (CAC), iliyoanzishwa miaka 20 iliyopita na Dr. Kedmon E. Mapana ambaye sasa ni Katibu Mtendaji wa BASATA, inaendelea kuwa
jukwaa la kukuza vipaji vya vijana, watoto na wanawake, kutangaza utalii wa kiutamaduni, na kuhimiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia sanaa na utamaduni.
Mbali na burudani, tamasha hili limekuwa fursa kwa mashirika ya Serikali, kampuni binafsi, wajasiriamali na wafanyabiashara kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa kwa jamii.
![]() |
Maandalizi ya Tamasha hilo mwaka huu 2025 |
0 Comments