Header Ads Widget

MKOA WA KATAVI KUANZA KUVUNA MATUNDA BIASHARA YA KABONI


Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma

Mkoa wa Katavi umeanza kuvuna matunda ya biashara ya kaboni (hewa ukaa), ambayo sasa imekuwa chanzo kipya cha mapato kinachochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. 

Akizungumza Julai 3, 2025 jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko, alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, mkoa umepokea zaidi ya Shilingi bilioni 25 kupitia biashara hiyo. Fedha hizo zimeelekezwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, kilimo, miundombinu, ajira na huduma za kijamii.


 Katika sekta ya elimu, mkoa umefanikiwa kujenga zaidi ya madarasa 50, kukarabati madarasa 20 na kujenga nyumba sita za walimu. Madawati takribani 1,500 yametolewa katika shule mbalimbali, shule mpya 129 zimejengwa kupitia programu za Serikali ikiwemo BOOST, UVIKO na SEQUIP, huku shule maalumu ya wavulana kanda ikipokea zaidi ya Sh bilioni 4 sawa na shule maalumu ya wasichana katika Halmashauri ya Nsimbo.

Mrindoko alieleza kuwa katika sekta ya afya, vichomea taka na mashimo ya kondo la mama yamejengwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma. Aidha, miradi 22 ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali mpya za wilaya inatekelezwa. Kaya zaidi ya 4,000 zimepatiwa bima ya afya, na chakula cha shule kimeendelea kutolewa kwa shule 16, huku walimu wa mkataba wakiendelea kuajiriwa.


Katika upande wa ajira na mazingira, zaidi ya vijana 100 wamepata ajira ya kulinda misitu, na wanawake wajasiriamali wamenufaika kwa kupatiwa mikopo ya zaidi ya Shilingi milioni 100. Mrindoko aliongeza kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 2 zilizopokelewa mwezi Aprili mwaka huu zinatarajiwa kutumika kuboresha shule za msingi na sekondari, kuongeza ajira kwa walimu na wahudumu wa afya pamoja na kuimarisha uhifadhi wa misitu.

Kwa upande wa kilimo, Mkuu huyo wa mkoa alisema ukarabati wa skimu kubwa za umwagiliaji za Mwamkulu na Kabage unaendelea kwa gharama ya takribani Shilingi bilioni 55. Mradi huo ambao kwa sasa umefikia robo ya utekelezaji, unatarajiwa kuongeza mara mbili eneo la umwagiliaji na kukuza uzalishaji wa mpunga kwa kiwango kikubwa. Zaidi ya vijana 700 wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa huku vyama vya ushirika vikiongezeka kwa kasi.


Katika miundombinu, barabara kuu zinazounganisha Mpanda na Tabora, Mpanda–Vikonge na Mpanda–Sitalike zimekamilika na zinatumika. Barabara za Vikonge–Luhafwe na Kibaoni–Sitalike zinaendelea kujengwa. Aidha, daraja kubwa la Kavuu linaendelea kujengwa, wakati daraja la Msadya tayari limekamilika na lipo katika matumizi.

Mradi mkubwa wa maji wa Miji 28 unaendelea kutekelezwa katika Manispaa ya Mpanda, na katika sekta ya nishati, vijiji vyote 172 vya mkoa huo vimeunganishwa na umeme kupitia Mradi wa REA, huku zaidi ya vitongoji 500 kati ya 912 vikiwa vimepata huduma hiyo muhimu

Mkuu huyo wa mkoa pia alibainisha kuwa miradi mingine mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Karema, ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya za Tanganyika na Mlele, ujenzi wa vihenge na ofisi za kuhifadhi mazao ya NFRA pamoja na ukarabati wa reli ya Kaliuwa–Mpanda yenye urefu wa zaidi ya kilomita 200.

Akihitimisha, Mrindoko alisema mafanikio hayo makubwa yanatokana na matumizi sahihi ya mapato ya kaboni, ushirikiano mzuri wa wananchi na uongozi makini wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya kweli na endelevu kwa Watanzania





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI