Header Ads Widget

KIBONDO YATUHUMIWA UBADHIRIFU FEDHA ZA MITIHANI

             Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma John Mgallah

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

HALMASHAURI ya wilaya Kibondo mkoani Kigoma inakabiliwa na tuhuma za kufanya malipo yasiyozingatia miongozo ikiwa ni posho  ya mitihani ya darasa la saba kwa watu mbalimbali waliokuwa wakisimamia mitihani hiyo ambapo malipo hayo yamejenga tuhuma za ubadhirifu.

Naibu Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma, John Mgallah alisema hayo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utendaji na utekelezaji wa mambo mbalimbali ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Mwezi April hadi juni mwaka huu ambapo jumla ya chambuzi za mifumo 15 zilifanyiwa kazi.

Mgallah alisema kuwa tuhuma hizo zinafuatia uchambuzi wa mifumo uliofanywa na taasisi hiyo ambapo imebaini kuwa kulikuwepo na malipo ya posho kwa watumishi wa halmashauri hiyo waliokuwa wakihusika na usimamizi wa mitihani hiyo  ambapo malipo hayakuzingatia miongozo ya fedha na maalipo kwa kazi hiyo.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa katika hatua ya awali wametoa ushauri kwa uongozi na  idara ya fedha ya halmashauri hiyo kuzingatia  sheria na miongozo ya fedha ili jambo hilo  lisijirudie lakini pia baadaa ya hatua shauri hilo linapelekwa idara ya uchunguzi ili kulifanyia uchunguzi na kuchukua hatua kwa wahusika.

Akitoa maelezo kwa njia ya simu kuhusiana na tuhuma hizo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kibondo, Diocles Rutema alisema kuwa bado hajapata taarifa hizo na kwamba atakuwa tayari kutoa maelezo yake na ufafanuzi wa jambo hilo atakapopata taarifa hiyo.


 




                          

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI