Mwongoza watalii wa Hifadhi ya Taifa ya Saadan Bagamoyo, Fred Nesto akionyesha kaburi la kiongozi wa Wamisionari, James Ledman aliyefariki dunia mwaka 1892 na kuzikwa katika eneo hilo.
NA ARODIA PETER
Kaburi ni mahali pa kulaza maiti ya binadamu au mabaki yake. Ni kumbukumbu ya waliotangulia mbele ya haki. Makaburini hapachezewi.
Watu wengi huogopa makaburi, ingawa baadhi ya jamii za waafrika huyatumia makaburi kufanya ibada za asili na matambiko. Kwa ujumla eneo la makaburi lina heshima yake.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani inayo makaburi ya kihistoria ya malikale na ni moja ya kumbukumbu na kivutio cha utalii nchini.
Makaburi hayo yapo katika Kijiji cha Saadani ambacho ni sehemu ya hifadhi, yametajwa kuwa ni miongoni mwa wamisionari wa kwanza ambao walifika ukanda wa pwani kwa ajili ya kueneza Ukiristo.
Historia inaeleza kuwa maeneo ya ukanda wa pwani mwanzoni yalitawaliwa na utawala wa kisultani ambao ulieneza dini ya kiislam kabla ya miaka ya 1880 walipokuja wamisionari wa kijerumani. Hata hivyo, hawakufanikiwa kwani utawala wa Sultani ulikwishaeneza Uislamu kwenye ukanda huo.
Akitoa maelezo ya makauri hayo hivi karibuni, mwongoza watalii wa Hifadhi ya Saadani, Fred Nesto anasema eneo hilo lina makaburi saba ya wamisionari wa kijerumani ambao waliuawa na utawala wa kisultani miaka ya 1892 na kuzikwa eneo hilo.
"Katika kijiji cha Saadani ambacho kipo karibu na hifadhi yetu ya taifa Saadani kina makaburi ya kihistori ambayo tunayaita ni mali kale,
“Makaburi haya ni miongoni mwa wamisionari saba wa kijerumani ambao waliingia maeneo haya ya pwani kwa ajili ya kutangaza dini ya Ukiristo katika kijiji hiki na maeneo jirani,
“Lakini hawakufanikiwa sana kutangaza ukiristo kutokana maeneo haya yalikuwa chini ya utawala wa sultani ndio maana kijiji hiki cha Saadani watu wengi waliopo hapa ni Waislam”anasema Nesto.
Aidha Nesto anaeleza kuwa wamisionari waliozikwa kwenye makaburi hayo, James Redman ambaye alikuwa kiongozi kutoka Taasisi ya Sociaty Mission crust iliyokuwa ikiwasaidia kufika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutangaza neno la Mungu.
Mwingine ni W.Siege aliyekuwa msaidizi wake pamoja na askari waliokuwa walinzi wao wakati wakifanya kazi ya kueneza neno la Mungu kwa watu.
Historia inaeleza kuwa, uamuzi wa kuwazika wamisionari hao katika Kijiji cha Saadani ulitokana na kutokuwapo mawasiliano ya usafiri wa ndege za masafa marefu kufika kwenye mataifa yao.
Makaburi hayo yamebaki kuwa kivutio cha mali kale katika hifadhi ya Saadani.
Mbali na makaburi, vivutio vingine ni mti wa mbuyu uliokuwa unatumika kutoa adhabu ya kunyonga watumwa ambao walionekana ni wazee, watukutu na wakaidi.
Pia kuna jengo lililokuwa linatumika kama soko la kuuza na kununua watumwa.
Shilawadu
Sherehe na ngoma za utamaduni ni moja ya burudani za wakati wa kijiji cha Saadani. Hizo hutumika kuwakutanisha kujadili na kutafakari mambo mbalimbali kuhusu siasa, ndoa na utamaduni. Vikao hivi vinajulikana kwa wakazi wa eneo hilo kama Shilawadu.
“Kwenye shilawadu maa nyingi hushirikisha wanaume ambapo hujadili mambo mengi yanayosaidia watu kujua historia ya taifa, chimbuko la dini zetu, utamaduni wa watu wa pwani na kujenga uzalendo.
“Ni vyema kila mtanzania afike katika hifadhi ya taifa saadani kwa ajili ya kujifunza na kufurahia maajabu ya kihistori na vivutio vilivyopo katika hifadhi hii ya Saadani”anasema Nesto.
0 Comments