Header Ads Widget

ISLAMIC STATE YADAI KUHUSIKA NA SHAMBULIZI DHIDI YA RAIA DRC

 


Wanamgambo wa kundi la Islamic State (IS) wametangaza kuhusika na shambulio lililotokea mwishoni mwa wiki katika mji wa Komanda, jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo takribani watu 45, wakiwemo waumini wa kanisa, waliuawa.

Shambulizi hilo linadaiwa kutekelezwa na kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF), lenye uhusiano wa moja kwa moja na IS, likiwa ni moja ya mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo kwa miezi ya karibuni.

Kwa mujibu wa Padre Dieudonné Beringa, Kasisi wa Parokia ya Bienheureuse Anuarite ambako mauaji yalifanyika, tukio hilo lilianza majira ya saa 1 asubuhi hadi saa 4 asubuhi ambapo milio ya risasi na moto wa nyumba ulisikika.

"Watu wenye silaha na mapanga waliwashambulia wanawake na wanaume waliokuwa kwenye ibada ya mkesha. Ni baada ya tukio ndipo tulipogundua ukubwa wa mauaji," alisema Padre Beringa.

Taarifa ya jeshi la FARDC imesema kuwa wanamgambo wa ADF waliwaua waumini hao kwa mapanga wakidai kuwa ni kulipiza kisasi kufuatia hasara waliyoipata kutoka kwenye operesheni ya pamoja inayotekelezwa na Jeshi la DRC na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).

Tangu mwaka 2021, operesheni hiyo ijulikanayo kama "Shujaa" imekuwa ikilenga kusambaratisha kambi za ADF zinazopatikana kwenye misitu ya mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini.

Taarifa ya jeshi imeeleza kuwa magaidi hao waliweza kujipenyeza kwenye mji huo kwa msaada wa baadhi ya wakazi, na hivyo limewataka wananchi wote waache mara moja ushirikiano wowote na adui.

Shirika la habari la Actualite, limeripoti kuwa waathirika wa shambulizi hilo ni pamoja na watoto tisa waliokuwa miongoni mwa waumini waliokuwepo kwenye ibada ya usiku.

Kwa upande mwingine, Marekani kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje imethibitisha kuwa IS iliitangaza ADF kuwa mshirika wake rasmi mwishoni mwa mwaka 2018, na imekuwa ikidai kuhusika na mashambulizi ya ADF tangu Aprili 2019.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI