Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko yaliyotokea katikati mwa jimbo la Texas, Marekani siku ya Ijumaa sasa imepanda zaidi 100 na idadi isiyojulikana ya watu hawajulikani walipo.
Vikosi vya utafutaji na uokoaji vinapita kwenye kingo za mito iliyojaa matope huku kukiwa na mvua na ngurumo katika eneo hilo, na matumaini yanazidi kufifia ya kupata manusura wengine, siku nne baada ya janga hilo.
Camp Mystic, kambi ya mapumziko kwa wasichana wa kikristo, imethibitisha kuwa wasichana 27 na wafanyakazi ni miongoni mwa waliokufa. Wasichana kumi na mshauri wa kambi bado wamepotea.
Wakati huo huo Ikulu ya Marekani imekataa hoja kwamba kupunguzwa kwa bajeti katika Huduma ya Kitaifa ya Hali ya Hewa (NWS) kumechochea kutatizika kwa juhudi za haraka za uokozi.
Takriban 84 kati ya waathiriwa - watu wazima 56 na watoto 28 - walikufa katika Kaunti ya Kerr, ambapo Mto Guadalupe ulijaa maji kutokana na mvua kubwa kabla ya siku ya Ijumaa.
Watu wazima 22 na watoto 10 bado hawajatambuliwa, imesema ofisi ya Polisi ya kaunti.
Wakosoaji wa utawala wa Trump wamehusisha janga hilo na kupunguzwa kwa maelfu ya wafanyakazi wa NWS.
Ofisi ya NWS inayohusika na utabiri katika eneo hilo ilikuwa na wafanyakazi watano waliokuwa zamu wakati dhoruba za radi zikitokea Texas Alhamisi jioni.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt alipinga majaribio ya kumlaumu rais. "Hiyo ilikuwa ni mipango ya Mungu. Sio kosa la utawala kwamba mafuriko yametokea, kulikuwa na maonyo ya mapema, shirika la Kitaifa ya Hali ya Hewa ilifanya kazi yake."
0 Comments